Home » » DC KOROGWE AAGIZA TAKUKURU ICHUNGUZE MIRADI

DC KOROGWE AAGIZA TAKUKURU ICHUNGUZE MIRADI


Na Mwandishi Wetu, Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Korogwe, kwenda kufanya tathimini ya miradi ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu katika Kata ya Shemshi, ofisi ya kata, choo cha soko pamoja na matumizi ya fedha za Serikali katika miradi mingine ya maendeleo iliyofanyika katika kata hiyo.

Agizo hilo alilitoa wilayani hapa juzi alipozungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Shemshi. 

Pamoja na mambo mengine, alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), viongozi wa mitaa wa kata hiyo pamoja na wananchi, kuonyesha wasiwasi juu ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika kata hiyo.

Katika mazungumzo yake, Gambo aliwaeleza wananchi kuwa, miradi hiyo ambayo hata yeye ameitembelea na kuona utekelezaji wake, haionyeshi kutekelezwa kama ilivyokuwa ikitarajiwa.

Alisema maelezo yaliyotolewa na Diwani wa Kata hiyo, Lazuli Shemahombwe, hayaridhishi na kuna haja TAKUKURU wakafika katika kata hiyo kuchunguza miradi hiyo.

“Mheshimiwa diwani, mimi mwenyewe nimejionea hiyo miradi na mimi ni Muislamu na nimefunga na moja kati ya msimamo wangu ni kutosema uongo. Kwa hiyo, ili ukweli ujulikane, naagiza TAKUKURU waje kufanya uchunguzi katika miradi hii.

“Mimi kama msimamizi wa shughuli za Serikali, siwezi kuona fedha za umma zikitumika vibaya na nikakaa kimya wakati wananchi wangu wanaendelea kupata tabu kutokana na vitendo vya ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Kwa maana hiyo, ngoja uchunguzi ufanyike ukweli ujulikane badala ya kuendelea kuamini maneno yako matamu,” alisema Gambo.

Awali, kabla ya kufanyika mkutano huo wa hadhara, mkuu huyo wa wilaya pamoja na Mbunge wa jimbo hilo, walitembelea na kujionea ujenzi wa choo cha soko, uchafuzi wa Mto Shemshi, ujenzi wa nyumba ya mwalimu pamoja na ofisi ya kata.

Akizungumza katika mkutano huo, Ngonyani, alisema wakati umefika kwa viongozi katika wilaya hiyo pamoja na kata hiyo kuwa wazi katika masuala ya mapato na matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo.

Alisema baadhi ya viongozi wana tabia ya kuficha taarifa hizo kwa wananchi jambo ambalo limekuwa likileta mitafaruku katika jamii hasa pale uwazi katika upatikanaji wa taarifa za mapato na matumizi zinapokosekana.

“Jamani tuache tabia za kutaka kuabudiwa na wananchi ndipo tutoe taarifa bali tuwe wakweli na wawazi katika suala la mapato na matumizi ya miradi yetu,” alisema Ngonyani.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa