Home » » Mahabusu 12, Mfungwa watoroka Gerezani Tanga

Mahabusu 12, Mfungwa watoroka Gerezani Tanga


Na Amina Omari, Lushoto
JESHI la Polisi mkoani Tanga, linawatafuta mahabusu 12 na mfungwa mmoja, baada ya kutoroka katika Gereza la Wilaya ya Lushoto usiku wa kumkia jana.

Akizungumza na MTANZANIA mjini hapa jana, Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, DSP Editha Mallya, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi wa kina umeanza ili kubaini mahabusu hao namna walivyotoroka.
Alisema mahabusu hao, walitoroka saa 8.25 usiku, baada ya kuchimba choo wanachotumia wafungwa hao na kupata upenyo wa kutokea.

“Tunakiri tukio hili, limetokea usiku wa kumkia jana, baada ya mahabusu 12 na mfungwa mmoja kuvunja eneo la choo na kutoroka… naomba uzungumze na makao makuu watakueleza vizuri,” alisema DSP Mallya. 

Alisema baada ya kufanikiwa kuchimba choo hicho, wafungwa hao, walitokea upande wa pili wa gereza na kutokomea kusikojulikana.

Alisema baada ya askari kupita kufanya ukaguzi, walibaini mahabusu wote na mfungwa mmoja, kuwa hawamo ndani.

Alisema mpaka jana mchana, hakuna mfungwa hata mmoja aliyekuwa amekamatwa na oparesheni ya kuwasaka inaendelea.

Naye Msemaji wa Jeshi la Magereza Makao Makuu, Omar Mtiga, alipoulizwa jana, alikiri kutokea kwa tukio na kusema “ni kweli ndugu hayo unayosema yametokea, hivi sasa nipo njiani kuelekea Lushoto ili kuungana na wenzangu kufanya uchunguzi.

“Nimeambiwa mahabusu 12 na mfungwa mmoja wametoroka, siwezi kujua mazingira yalikuwaje, vuta subira tutawataarifu hali halisi ya jambo hili… kwa vile kule ni milimani nitachelewa leo kuwaeleza, lakini naamini kesho (leo), nitakuwa katika nafasi nzuri,” alisema Mtiga.

Juhudi za MTANZANIA kumpata Mkuu wa Usalama wa Jeshi la Magereza Tanzania, Kamishina Mboya hazikufanikiwa, baada ya simu yake ya kiganjani kuita muda mrefu. 

Kwa upande wake, Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Tanga, Rajab Mohamed, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kusema jeshi hilo kwa kushirikiana na Magereza, wametumwa askari wengi kwa ajili ya kuendesha msako.

“Ndugu yangu, taarifa nilizonazo ni kwamba tukio hili limetokea, sasa tumetuma askari wetu na wale wa Magereza eneo la tukio ili tujue chanzo cha suala hili,” alisema Mohamed.

Alisema hivi sasa, wanawasiliana na wenzao wa Lushoto ili kupita maeneo mbalimbali kuendesha msako.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa