Salim Mohammed, Tanga
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Tanga imewafikisha mahakamani watu watatu kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka na kushindwa kukamilisha ujenzi wa mfereji ambao ulikuwa umefadhiliwa na Tasaf.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana baada ya kusainiwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa, Edson Makallo iliwataja watu hao kuwa ni Julius Kahangi, Bonna Aloyce na Salim Amir ambao wote ni wakazi wa Jiji la Tanga.
Taarifa hiyo ilisema kuwa watu hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka kwa kushindwa kufanya ukaguzi wa kina wa ujenzi wa mifereji ya maji katika Mtaa wa Azimio jijini hapa ambao ulikuwa ukifadhiliwa na Tasaf.
Ilisema watu hao walishindwa kusimamia ujenzi wa mfereji ulioko Mtaa wa Azimio huku wakitumia madaraka yao vibaya na kuisababishia Serikali hasara hasa wao wakiwa viongozi mbele ya jamii.
Taarifa hiyo ilimtaja Julius Kahangi kuwa ni fundi Sanifu wa Hamlashauri ya Jiji la Tanga huku Bonna Aloyce Mtui akiwa Mhandisi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) na Salim Amir Faki akiwa ni Mkamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mtaa Azimio.
Taarifa hiyo ilisema kuwa Februari mwaka 2008, watu hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza wajibu wao wa kazi kama mikataba yao ilivyoainishwa na badala yake ikaisababishia hasara Serikali.
Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilitoa wito kwa wananchi kuwafichua wala rushwa pamoja na wapokeaji ili kuiwezesha jamii kupata huduma stahiki pasina kupita njia za panya lengo likiwa ni kuisaidia Serikali katika juhudi zake za kuwaletea maendeleo watu wake.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment