Home » » Wakulima wa mkonge walalamikia ubaguzi

Wakulima wa mkonge walalamikia ubaguzi


Burhani Yakub, Tanga yetu

WAKULIMA wadogo wa mazao ya Mkonge na Chai nchini, wamesema kuna baadhi ya wakubwa ambao wamekuwa wakifanya njama za kuwadhoofisha ili wasimudu kuendesha kilimo hicho na wameiomba Serikali kuingilia kati.

Wamesema licha ya kuwa nchi nyingi Duniani zimeanza kuingia katika
mapinduzi ya kilimo cha wakulima wadogo, lakini kuna baadhi ya waliopo
kwenye mazao ya mkonge na chai wamekuwa wakipigwa vita.

Mwenyekiti wa wakulima wadogo wa mashamba ya Mkonge ya Mwelya Wilayani Korogwe, Fredrick Maliki alisema pamoja na kwamba wamejitahidi kuendesha kilimo hicho baada ya kukabidhiwa mashamba na kampuni ya
Katani Limited kuna baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiwawekea vikwazo ili wakate tamaa.

Alisema wakulima wadogo wa Mkonge waliopo mashamba ya Mwelya wamepata mafanikio makubwa kutokana na moyo wao wa kuliendeleza zao hilo ambapo hivi sasa wanazalisha mkonge mwingi lakini kuna mambo mengi yanayofanyika ili wakate tamaa.

“Tatizo hapa kuna wakubwa ambao hawataki sisi wakulima wadogo tuendeshe mashamba haya, bado wana mawazo mgando kwamba kilimo hiki hakiwezi kuendelea  bila wakulima wakubwa wenye esteti na
manamba,” alisema Maliki na kusisitiza kuwa mambo hayo yameshapitwa na
wakati.

Alisema kama Serikali haitaingilia kati na kuwasaidia wakulima wadogo, kuna hatari ya kuyumbishwa na maendeleo yaliyoanza kupatikana sasa yatavurugwa kwa sababu ya njama za wakubwa.

Naye Mwenyekiti wa wakulima wadogo wa zao la Chai nchini (TASTGA), George Kyejo alisema umefika wakati kwa Serikali kutupia macho vikwazo wanavyokabiliana navyo ambavyo vingi vinatokana na njama
za kuwadhoofisha.

Alitaja miongoni mwa njama hizo ni kuchochea migogoro kwenye mashamba
na viwanda vinavyomilikiwa na wakulima wadogo wa chai ili visiweze kujiendesha hatimaye wakubwa wavichukue.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa