Home » » DC: Tumieni fursa kujiletea maendeleo

DC: Tumieni fursa kujiletea maendeleo


Salim Mohammed, Tanga
MKUU wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendega amewataka madereva wa Bodaboda na Bajaj, mkoani humo kutumia fursa za mikopo zilizopo kwa vijana ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta maendeleo maeneo wanayoishi.

Dendega alitoa rai hiyo jana katika hafla ya utoaji vyeti kwa wahitimu wa mafunzo ya udereva wa  Bodaboda na Bajaj mkoani Tanga, yaliyoendeshwa kwa siku sita na Shirika la Ant-Porvety Enveronmental Care (APEC) lenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa kila mwaka Halmashauri ya Jiji la Tanga hutenga fungu kwa ajili ya mikopo kwa vijana ambalo moja ya malengo yake ni kuwawezesha vijana kujishughulisha na kazi za ujasiriamali ili kuepuka na vishawishi vya ulevi na wizi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ingawa fungu hilo limekuwa likitengwa na kuidhinishwa kila mwaka na Baraza la Madiwani, kwa lengo la kuwawezesha vijana kujikomboa dhidi ya umaskini,  lakini la kushangaza vijana wengi hawajui kuwepo kwa fungu hilo.

“Madereva wa Bodaboda, Bajaj na ninyi vijana wenzangu, hivi munajua kuwa halmashauri imetenga fungu kwa ajili yenu?" alihoji Dendega akiongeza: 
"Hebu itumilieni fursa hii ili, wale ambao bado hawajamiliki Bodaboda zao wamiliki, nami nitakuwa balozi wenu." 
Alisema madereva wa Bodaboda na Bajaj ni watu muhimu katika sekta ya usafirishaji ambao pia wanaweza kufanya ujasiriamali, hivyo kustahili pia kupata mafunzo ya ujasiriamali na kupewa fursa za mikopo katika taasisi za fedha.

Dendega alisema mafunzo hayo yatawawezesha kufanya kazi zao kitaalamu, kuweza kutoa ajira ndogondogo na kusaidia kupunguza umaskini katika maeneo yao.

Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi wa APEC, Respicias Timanywa alimuomba Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Abdi Isango, kuwachukulia hatua za kisheria waendesha Bodaboda na Bajaj ambao hawajapata elimu ya udereva.

Alisema kuna waendeshaji wengi wa Bodaboda na Bajaj na ambao wako na leseni zao lakini hawajapitia mafunzo ya kujua sheria za alama za barabarani na kuwa chanzo cha kuongezeka kwa ajali na vifo.

Alisema kufanya hivyo kutapelekea kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo na ajali zinazosababishwa na madereva hao ambao hawajapitia mafunzo hayo na hivyo kutishia uhai wa Sekta ya usafirishaji hasa Bodaboda.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa