Mashaka Kibaya, Muheza
MKUU wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu amewataka wakulima wa wilaya hiyo kuachana na kilimo cha mazoea kwa kushiriki kilimo cha mazao ya aina moja yanayochukua muda mrefu na kuwahimiza kulima zao la ufuta ili kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Mkuu huyo wa wilaya pia, aliwahakikishia wakulima hao kuwa, jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kilimo cha zao la mpira kinafufuliwa wilayani humo kama zao mbadala litakalosaidia kuimarisha ukuaji uchumi wa mtu mmoja mmoja na halmashauri kwa ujumla.
Mgalu alitangaza mikakati hiyo juzi, alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu jitihada zinazopaswa kufanyika ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Wilaya ya Muheza kupitia sekta ya kilimo, akiwataka wakulima kuangalia uwezekano wa kubadilika.
Mgali alisema, kwa sasa wananchi wa wilaya hiyo wamejikita zaidi katika kilimo cha mahindi na zao la machungwa,licha ya kuwapatia tija inawachukua muda mrefu kuonja mafanikio ambapo kama wangelima ufuta wangenufaika kwa haraka.
Alisema kwa sasa zao la ufuta lina bei nzuri na kuwataka wakulima kutilia mkazo kilimo cha zao hilo ili liwasaidie kuongeza kipato chao na kujikwamua katika umasikini uliokithiri miongoni mwao.
“Mimi binafsi siku moja nikiwa kama mwanamama nilijaribu kupita sokoni na kuuliza bei za vitu mbalimbali na nilipofika kwenye ufuta nikakuta una bei kubwa sana,hivyo ufuta kama utalimwa kwa wingi utasaidia kubadilisha maisha ya wananchi", alisema Mgalu.
Akizungumzia zaidi kilimo cha zao la mpira ambacho kipindi cha nyuma kilisaidia kuharakisha maendeleo katika wilaya hiyo ya Muheza,Mgalu alisema tayari utaratibu wake ulishaandaliwa na mkuu wa wilaya aliyepita na hivyo mikakati iliyopo ni kuiendeleza.
Alisema kwamba tangu alipoanza kazi rasmi wilayani humo, ameshafanya ziara maeneo mbalimbali na kusikiliza kero za wananchi ambapo pia alitumia fursa ya mikutano aliyojumuika na wakazi hao kuwashauri mambo mbalimbali kuhusu maendeleo yao.
Alisema kwa dhati wa moyo wake katika nafasi aliyonayo, atajitahidi kuitumikia kikamilifu akishirikiana na wananchi hao kutatua kero zilizopo huku akielezea kuridhishwa kwake na ushirika wa wakulima Kilongo kwa kuamua kujiunga pamoja ili kuweza kusaidiwa kirahisi.
Kuhusu zoezi la Sensa ya watu na makazi, mkuu huyo alisema kuwa, utaratibu wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi ili washiriki kikamilifu unaendelea , ambapo wameanza kupata uelewa juu ya umuhimu wa mpango huo wa Serikali yao.
''Kwa ujumla elimu imeendelea kutolewa kwa kasi ya aina yake ambapo tumewatembelea wananchi kule waliko,sensa ni zoezi muhimu sana hivyo sasa wanaonekana kuelewa kwani mipango ya serikali kwa wananchi wake itafanikishwa kwa zoezi hili", alisema Mgalu.
Aidha mkuu huyo wa wilaya alibainisha kwamba ziara za kutembelea maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Muheza, zitaendelea kufanyika kuhakikisha kwamba anakutana na wananchi na kujua matatizo yao ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment