Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema
hadi kufikia keshokutwa atakuwa ameshapewa orodha kamili ya viwanda
vinavyotakiwa kunyang’anywa.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli
kuoneshwa kushangazwa na kukerwa na kitendo cha waziri huyo, kuchelea
kuwanyang’anya umiliki wa viwanda wawekezaji walioshindwa kuviendeleza
tangu walipobinafsishiwa miaka 20 iliyopita.
Dk Magufuli alitoa agizo hilo la kunyang’anywa kwa viwanda hivyo
wakati akiwa kwenye ufunguzi wa kiwanda cha saruji cha Kilimanjaro, Kata
ya Maweni jijini Tanga juzi. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, nchi nzima
ina viwanda 197 vilivyotelekezwa baada ya kubinafsishwa takribani miaka
20 iliyopita, vikiwemo viwanda vilivyopo mkoani Tanga. Kutokana na kauli
hiyo ya Rais, Mwijage amesema hadi kufikia hiyo keshokutwa Alhamisi
atakuwa ameshapata orodha kamili ya wanaotakiwa kunyang’anywa viwanda
vyao, na siku inayofuata atayaweka wazi majina hayo.
Mwijage alisema makatibu wakuu wa wizara zote, ambazo kwa namna moja
au nyingine zinahusika na viwanda, watakutana kuzungumzia wawekezaji
huku pia wakuu wa mikoa wote nchini nao watashirikishwa. Alisema kwa
kuwa yeye ni waziri anayeshughulikia viwanda, anatambua kuwa kuna
viwanda ambavyo vipo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na
wizara nyinginezo kwa hiyo ana wajibu wa kusikia kutokea wizara hizo.
Alibainisha kuwa kwa kuwa viwanda vingine vipo mikoani, ameona kuwa
kuna haja ya kuwashirikisha wakuu wa mikoa kwa kuwa wao ndiyo wenyeviti
wa Kamati za Ulinzi na Usalama wanaweza kumhakikishia viwanda
vilivyoshindwa kuendelezwa na kama viliuzwa kweli kwa wawekezaji.
Alisema kwa wawekezaji watakaonyang’anywa viwanda, hawatalipwa fidia ya
aina yoyote ile kwa kuwa kwa miaka 20 wamepewa viwanda na wameshindwa
kuviendeleza badala yake wamevitumia kama dhamana ya kuchukulia mikopo
benki.
“Najua nimeshamuomba Rais kuwa asinikumbushe tena kwa kuwa kwanza
nilishaambiwa kushughulikia suala hili na nikawa kidogo nalifuatilia
kikawaida ila kwa sasa sina tena huo muda wa kuwabembeleza,” alieleza
waziri huyo. “Kwa kawaida ukishindwa kumbwekea mtu utajikuta unabwekewa
wewe na mimi nakwambia hiyo Ijumaa nitabweka ni kuwanyang’anya tu.”
Alifafanua kwamba wakati mwingine alikuwa akikwazwa na watu ambao
wakati akiwaeleza kuhusu kuviendeleza, wakawa na visingizio vya kuwa na
kesi mahakamani. Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani
ilianza kuhimiza uanzishwaji wa viwanda na wapo Watanzania walioitikia
kwa kuanzisha, lakini wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua maeneo na
kuimarisha miundombinu ili hali wanaweza kupewa hivyo vilivyoshindwa
kuendelezwa na mwekezaji na wakaviendeleza.
“Kuna mtu ana kiwanda Chalinze cha vigae amelazimika kuvuta maji
kutokea mto Ruvu hadi Chalinze, kuvuta umeme takribani kilometa mbili
kuelekea kwenye eneo la kiwanda chake, sasa mtu huyu anaingia gharama
kubwa wakati watu kama hawa wakipewa kiwanda kilichotelekezwa na
mwekezaji na kipo mazingira yenye miundombinu bora si anafanya kazi
vema,” alieleza Mwijage.
Mbunge huyo wa Muleba Kaskazini mkoani Kagera, alisisitiza kuwa
anaelewa kuwa Rais Magufuli bado ana imani naye na kuwa kama ni alama
katika utendaji wake kwa wizara hiyo, anaweza kujipatia asilimia 60 ya
uwezo kwa hiyo hatokubali mtu kumwangusha.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment