Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(kulia) akijibu kero mbalimbali za uhifadhi kwa wananchi wa Kijiji cha Shume
Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya
kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(wa pili kushoto) akisikiliza moja ya kero kuhusu uhifadhi kutoka kwa Abunio
Abraham Shangali (wa pili kulia) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shume Nywelo,
Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya
kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani
(wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kikundi cha uhifadhi na utalii cha Friends
of Usambara kilichopo Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku
moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
NA HAMZA TEMBA - WMU
Katika kuhakikisha sekta ya utalii
nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha utalii wa Misitu
ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa tofauti na
ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.
Hayo yamesemwa jana wilayani Lushoto
na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa
kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro
mbalimbali ya uhifadhi.
Alisema sekta ya utalii nchini
imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu
ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na
ambavyo hupatikana Tanzania pekee.
“Tumezoea zaidi utalii wa
wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu
yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama
vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa kufanya ni
kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi
zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.
Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya
Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo
16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa fursa pana ya
kuendeleza sekta ya utalii nchini.
0 comments:
Post a Comment