Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Imeandikwa na Anna Makange, Korogwe
RAIS John Magufuli ameziagiza wizara za Fedha na Mipango na Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi kuandaa mapendekezo na kupeleka
bungeni mwaka huu marekebisho ya sheria yanayotaka kulipwa kwa Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) kwa miradi inayopata ufadhili kutoka kwa wadau
wa maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia.
Ametoa agizo hilo wakati akihutubia wananchi wa Korogwe waliohudhuria
ufunguzi wa stendi mpya ya kisasa ya mabasi iliyogharibu Sh bilioni nne
eneo la Kilole. Dk Magufuli alisema utaratibu huo unafanya serikali
kulipa VAT kwa serikali yenyewe jambo ambalo si sahihi kwa kuwa fedha
hizo zingetumika kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
Alitoa agizo hilo baada ya Naibu Waziri Tamisemi, Selemani Jaffo
kueleza kuwa ipo changamoto ya kisheria inayokabili miradi ya maendeleo
inayotekelezwa na serikali kutakiwa kulipa VAT na kusababisha serikali
kulipa fedha za ziada Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa sababu mikopo na
ruzuku kutoka kwa wafadhili hazitengi malipo ya kodi.
“Nawaagiza mawaziri wa wizara zote mbili kuandaa marekebisho ya
sheria hii ambayo ilipitishwa mwaka 2015 ili mwezi Septemba iweze
kurekebishwa bungeni... tunahitaji fedha, lakini sio kwa kila kitu
tutozwe VAT hiyo ni kujichelewesha hayo mambo ni ya ovyo lazima
tuyaache,” alieleza Dk Magufuli.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), January Makamba amemuomba rais kushughulikia mgogoro wa
kiwanda cha kusindika chai cha Mponde wilayani Lushoto ambao umechukua
muda mrefu na kusababisha wakulima wa Jimbo la Bumbuli wilayani humo
kushindwa kujiendeleza kiuchumi. Stendi iliyojengwa mjini Korogwe ni
miongoni mwa mradi 11 inayojengwa na kusimamiwa na Tamisemi kwa ufadhili
wa Benki ya Dunia katika baadhi ya halmashauri nchini.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment