Imeandikwa na Anna Makange, Handeni
RAIS John Magufuli ametoa wiki mbili kwa Mhandisi Mshauri pamoja na
Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa ujenzi wa mabwawa matatu ya maji safi
wilayani Handeni mkoani Tanga, kurudi mara moja katika eneo la ujenzi
ili kukamilisha kazi hiyo.
Pia amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba
kuwakamata wahusika hao ambao ni Kampuni za DON Consultant na TANSINO
endapo watashindwa kutekeleza agizo hilo. Ametoa maagizo hayo jana
wakati wa siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Tanga katika
mkutano wa hadhara, uliofanyika Kata ya Vibaoni mjini Handeni.
Dk Magufuli alisema haiwezekani wananchi wa Handeni, kuendelea
kusubiri maji kwa zaidi ya miaka mitano sasa wakati tayari serikali
imeshawalipa jumla ya Sh bilioni 2.8 kwa makandarasi hao, ambao alisema
wamefanya kazi ya ovyo. “Fedha ya serikali haipotei, huyu consultant
(mshauri) na contractor (mkandarasi) nawataka ndani ya wiki mbili wawe
wamerudi site (eneo la ujenzi), nataka waanze kuyachimba haya mabwawa
kwa fedha zao wenyewe na baada ya kukamilisha na kupata certificate
(cheti) ndipo tutawalipa shilingi bilioni moja na milioni mia mbili
zilizosalia,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza, “Najua ukubwa wa tatizo la maji hapa, hivyo wananchi wa
Handeni hawawezi kuendelea kusubiri maji kwa miaka mitano wakati fedha
ya serikali imeliwa na watu wachache, jambo hilo halikubaliki, Tanzania
siyo nchi ya kuliwa hela. Mimi mtumbua majipu nipo na wasipoenda
kukamilisha ujenzi huu haraka, basi yatawakuta yaliyowakuta wakandarasi
wazembe... endapo watakaidi agizo hili basi RPC Tanga nakuagiza uende
kuwakamata ili waende gerezani kwa sababu sheria ni msumeno.”
Mradi huo wa ujenzi wa mabwawa matatu ya maji katika miji ya Mkata,
Manga na Kwandugwa wilayani Handeni, ulipangwa kugharimu jumla ya Sh
bilioni 4.1. Hadi sasa tayari makandarasi wameshalipwa Sh bilioni 2.8
kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya kukusanya maji ya mvua pamoja na
miundombinu ya kusambazia, lakini haukukamilika kwa wakati na hivyo
kusababisha wananchi kuendelea kuteseka. Akiwa njiani kutoka Korogwe
ambako alizindua ujenzi wa stendi mpya ya mabasi, Rais Magufuli alitoa
msaada wa Sh milioni tano taslimu kwa Shule ya Msingi Misima kwa ajili
ya ujenzi wa vyoo vya shule hiyo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment