Na Joachim Mushi,
WAKULIMA wa Mradi wa utafiti wa mbegu bora chotara za mahindi
zinazostahimili ukame (WEMA), wilayani Handeni wameiomba Serikali
irekebishe sheria ya uzalishaji wa mbegu ili kutanua wigo wa uzalishaji
mbegu kupitia taasisi za Serikali kama vile Jeshi la Kujenga Uchumi
(JKT), Jeshi la Magereza pamoja na zinginezo zilizopo.
Wakulima
hao wametoa ombi hilo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakulima
Katika Kijiji cha Kabuku Ndani, kilichopo Wilaya ya Handeni mkoani
Tanga, kufuatia uwepo wa changamoto ya kutopatikana kwa uzalishaji wa
mbegu ya kutosha kulingana na mahitaji kama ile ya WE 2109 ambazo
zimeonekana kufanya vizuri zaidi maeneo ya Wilaya ya Handeni.
Akisoma
risala mbele ya mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Wakulima
hao, Costansia Msola alibainisha kuwa bei kubwa ya mbegu zinazozalishwa
na makampuni ya mbegu ulikuwa changamoto licha ya uwepo wa wadudu
waharibifu waliojitokeza kwenye mashamba ya wakulima na kukwamisha
matarajio ya uzalishaji.
Kwa
upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni,
aliyewakilishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, John Mahali
aliwapongeza kikundi cha wakulima 22 waliokubali kushirikiana na
watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa
kushirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kuendesha mradi wa
utafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame (WEMA)
ambao umeonesha mafanikio makubwa.
Aidha
aliwataka wakulima Wilayani Handeni kukubali mabadiliko na kuanza
kutumia mbegu hizo za kisasa zaidi ya aina 11 zilizoonesha mafanikio
makubwa katika utafiti. "...Huko nyuma tulikuwa tukitumia mbegu za asili
ambazo zilikuwa hazifanyi vizuri, naombeni sasa tutumie mbegu hizi bora
zilizofanyiwa utafiti na WEMA kwa kilimo bora," alisisitiza, Bw. John
Mahali akizungumza na wakulima.
Aliyaomba
makampuni ya uzalishaji mbegu kujitokeza na kufanya uzalishaji wa mbegu
bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame ili kuwasaidia wakulima
upatikanaji wake kwa wakulima.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti kutoka
Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, Jackson Nkuba akimwakilisha Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Utafiti alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na
makampuni yatakayojitokeza kuzalisha mbegu hizo bora kwa wakulima hivyo
kutoa rai kujitokeza kwa wingi.
Alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha mkulima anafanya kilimo cha kisasa
chenye tija apate mazao mazuri na yakutosha ambayo yatamletea maendeleo.
Alisema njia pekee ya kufanya vizuri kwenye kilimo ni kuendesha tafiti
mbalimbali na ndio sababu Serikali kwa kushirikiana na mashirika anuai
inaendelea kutoa fedha na kufanya tafiti tofauti.
Hata
hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe
akizungumza aliiomba Serikali kujenga viwanda vya kusindika Mahindi na
mazao mengine yanayozalishwa na wakulima wilayani humo ili wakulima
wanufaike zaidi na mazao hayo, tofauti na kutegemea kuuza nje ya eneo
hilo.
"Haiwezekani
mahindi tulime sisi tuyauze Dar es Salaam na mikoa mingine wayasindike
(unga) na kuja kuuziwa tena sisi wenyewe wakati mwingine kwa bei ya juu
tofauti na tulivyo uza siye...," alisema Bw. Mkufwe.
Mradi
wa utafiti wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame
(WEMA) ulianza mwaka 2009 ukiwa na lengo la kufanya utafiti shirikishi
wa mbegu bora chatara za mahindi zinazostahimili ukame kutokana na
mabadiliko ya hali ya hewa, ukiwa na mkulima mmoja tu lakini kwa sasa
una kundi la wakulima 22 ambao walihamasika na kujiunga pamoja
kushirikiana na watafiti.
0 comments:
Post a Comment