Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (kulia) akielekea katika Gati namba moja
la Bandari ya Tanga kuangalia shughuli mbalimbali zinazoendelea
bandarini hapo. Penmbeni yake ni Mhandisi wa Bandari hiyo Bw. Saleh
Sapi.
Mhandisi wa Bandari ya Tanga Bw.
Saleh Sapi (mwenye t-shirt) akitoa maelezo kwa Kaimu Katibu Mtendaji wa
Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (koti jekundu) juu ya kina cha
maji katika bandari hiyo. Upande wa kulia ni Bw. Jordan Matonya na Bi
Anna Kimwela, wachumi kutoka Tume ya Mipango. Upande wa kushoto (mwenye
miwani ya jua) ni Afisa Mipango Mwandamizi wa Bandari ya Tanga, Bibi
Moshi Mtambalike.
Shughuli za kupakia Magogo ya Umeme zikiendelea katika Bandari ya Tanga.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akikagua ukarabati wa boti katika Bandari ya Tanga.
Mhandisi wa bandari ya Tanga Bw.
Saleh Sapi akimueonesha Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi
Florence Mwanri ujenzi unaoendelea (hauonekani pichani) wa gati namba
mbili katika Bandari ya Tanga. Pembeni ya Mhandisi Sapi ni Mchumi Mkuu
kutoka Tume ya Mipango Bw. Aloyce Shayo na wa kwanza kulia ni Bw. Jordan
Matonya Kutoka Tume ya Mipango.
Ujenzi wa gati namba mbili ukiendelea katika Bandari ya Tanga.
PICHA ZOTE NA ADILI MHINA, TUME YA MIPANGO.
……………..
Na Adili Mhina, Tanga.
Mamlaka ya Bandari nchini
imeshauriwa kuangalia taratibu za kurasimisha bandari bubu ili kudhibiti
upotevu wa mapato ya Serikali pamoja na kuhakikisha bidhaa
zinazopitishwa katika maeneo hayo zinakubalika kisheria.
Ushauri huo umetolewa hivi
karibuni na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence
Mwanri wakati timu ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Tume ya
Mipango ilipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kwa lengo la kufanya
ufuatiliaji na tahmnini ya shughuli zinazotekelezwa bandarini hapo.
Mwanri alieleza umuhimu wa
kurasimisha bandari bubu baada ya kupata taarifa kuwa katika Mkoa wa
Tanga pekee kuna bandari bubu takriban 42 ambazo zinaendesha shughuli
mbalimbali bila ya usimamizi wa Mamlaka ya Bandari.
Mwanri alieleza kuwa kwa sasa
Serikali haiwezi kuendelea kufumbia macho suala hilo kwani licha ya
Serikali kupoteza mapato yake wapo baadhi ya watu wanaotumia njia hizo
nyakati za usiku kuendesha shughuli zinazoenda kinyume na kisheria na
taratibu za nchi, hivyo kuchochea uhalifu.
“Kuna umuhimu mkubwa kuangalia
shughuli zinazoendelea katika bandari bubu kwa kuwa wakati mwingine
wafanya biashara wanaopaswa kulipa kodi wanatumia maeneo hayo kupitisha
bidhaa bila kulipa kodi na wengine wanatumia bandari bubu kuendesha
biashara haramu. Ni lazima kuanza kufanya utaratibu wa kurasimisha
bandari hizo ili kuharakisha maendeleo ya nchi yetu,” alisema Mwanri.
Pamoja na hayo, Mwari alitembelea
maeneo ya Bandari ya Tanga na kushuhudia shughuli mbalimbali zikiendelea
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa gati namba 2 ikiwa ni moja ya malengo
katika kuimarisha huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini
hapo.
Awali, Mhandasi wa Bandari hiyo
Bw. Saleh Sapi alieleza kuwa Bandari ya Tanga inapokea tani laki mbili
za mizigo kwa mwezi ambapo bidhaa kubwa zinazoingizwa kutoka nje ni
malighafi ya kutengenezea saruji wakati bidhaa zinazosafirishwa kwenda
nje ni kahawa, mkonge, pamoja na mbao ambazo kwa sasa kibali chake
kimesitishwa kwa muda.
Mhandisi huyo alieleza kuwa
Bandari ya Tanga haina eneo lenye ukubwa wa kutosha kwa ajili ya
kutekeleza huduma zake kwa ufanisi huku kina cha maji kikiwa ni mita nne
kitu kinachopelekea meli kubwa kushindwa kufika kwenye gati za bandari
na badala yake matishari hutumika kubeba mizigo hiyo.
Mhandisi Sapi alifafanua kuwa
kutokana na changamoto hiyo nguvu kubwa inaelekezwa katika kuangalia
namna ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mwambani ambapo
kuna kina cha maji kinatosha kuhudumia meli kubwa na pia kuna eneo la
kutosha shughuli mbalimbali za bandarini.
0 comments:
Post a Comment