Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
SEKTA ya
kilimo inayojumuisha ukulima, ufugaji na uvuvi, imeendelea kuwa sekta
kiongozi. katika kutoa ajira na kuwa tegemeo la maisha kwa asilimia 75 ya Watanzania wanaoishi Vijijini.
Kujitosheleza
kwa chakula ni muhimu kwa usalama na utulivu wa nchi. Taarifa ya Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuwa kiwango cha kujitegemea kwa
chakula kimeongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2005 hadi asilimia 125 mwaka 2014.
Pamoja na uzalishaji kuwa mkubwa, inaelezwa kuwa kiasi kikubwa cha mazao ya nafaka yanayozalishwa nchini huharibika
na kupotea baada ya kuvunwa. Upotevu huo hutokana na matumizi ya mbinu
duni za kuhudumia mazao wakati wa uvunaji, usafirishaji na uhifadhi
kwenye maghala.
Uzalishaji
wa mazao ya nafaka unakadiriwa kufikia wastani wa tani 3, 897,500 kwa
mwaka na asilimia 80 ya nafaka huzalishwa na kuhifadhiwa vijijini,
ambapo hata hivyo uwezo mdogo na maghala duni yanayotumiwa na wakulima
vijijini wakati wa kuhifadhi huruhusu upotevu wa nafaka hadi asilimia
10.
Takwimu
za Shirika la Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonyesha kuwa,
asilimia 30 hadi 40 za nafaka zinazovunwa hupotea kila mwaka nchini.
Mahindi ni miongoni mwa mazao
makuu ya nafaka hapa nchini yanayolimwa nchini Huzalishwa kwa wastani
wa tani 2,393,000 kwa mwaka ambao ni sawa na asilimia 63 ya mazao yote
ya nafaka.
Takwimu
za Wizara ya Kilimio, Mifugo na Uvuvi zinaonyesha uzalishaji wa mahindi
unaongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2011 uzalishaji wa
mahindi katika nchi nzima ulifikia tani 4,341, mwaka 2012 tani 5,104 na
mwaka 2013 tani 5,174.
Taarifa
kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi zinaeleza kuna uwezekano mkubwa wa
kuharibika kwa tani 40,000 za mahindi yanayoendelea kununuliwa katika
msimu huu na Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kutokana na
uhaba wa maghala ya kuhifadhi.
Wakala
katika mikoa hiyo anakabiliwa na changamoto ya uwezo mdogo wa kuhifadhi
chakula hicho katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mahindi na
kusababisha akiba kubwa ya chakula kuhifadhiwa nje ya maghala.
Utafiti uliofanywa na mradi wa USAID Tuboreshe Chakula
umebaini kuwa kutokana na uhifadhi duni na mbinu bora za kilimo cha
mazao ya nafaka kama mahindi, alizeti na maharage unasababisha ukungu
kwenye mazao hayo hali inayosababisha sumu kuvu yenye madhara makubwa
kwa mlaji.
Mhadhiri
Mwandamizi wa chuo kikuu cha sayansi cha Nelson Mandela, Dk. Martin
Kimanya anasema sumu hiyo haiwezi kuondolewa kwa kupika chakula na
badala yake watumiaji wanapaswa kuchagua nafaka kwa kuondoa zile ambazo
zimebadilika rangi na kuwa na ukungu.
“Wakati
Tanzania ikiwa katika nafasi ya nne kwa ulizalishaji wa zao la mahindi
barani Afrika, imeelezwa kuwa watumiaji wa mahindi wanakula 30% ya sumu
kuvu inayotokana na uhifadhi duni wa mahindi” anasema Prof Kimanya.
Kutokana
na tatizo hilo mradi wa USAID tuboreshe chakula umeanza mikakati ya
kuinusuru jamii ikiwemo kwa kutoa elimu kwa wasindikaji wa vyakula
pamoja na wakulima ili kufahamu sumu kuvu na madhara yake.
Katika
kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula nchini, Serikali
kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula Nchini (NFRA) imepanga kujenga
maghala 275 kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la
mahindi.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa anasema Serikali imejipanga katika kuondoa tatizo
la upungufu wa chakula nchini kwa kujenga magala mengi zaidi ya
kuhifadhi chakula katika maeneo mbalimbali yenye changamoto za upungufu
wa chakula.
“Serikali kupitia
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala
ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa na kwa sasa ghala
moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi
Mkoani Mbeya ” anasema Majaliwa
Aidha
Majaliwa anasema Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka
Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90.
Anasema maghala
yanakayojengwa si kwa ajili ya kuhifadhi chakula tu bali hata kuweka
dawa kwa urahisi, kukausha, kuondoa unyevunyevu na kusafisha kwa kiwango
kinachohitajika.
Waziri
Mkuu anasema kuwa anasema ujenzi wa magahala hayo utaliongezea taifa
uwezo wa kuhifadhi chakula tofauti na hali ilivyo sasa.
Waziri
wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba anasema Serikali
imeiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) kununua mahindi
moja kwa moja kutoka kwa
wakulima na kuachana na mfumo wa zamani ambapo wakulima walikuwa
wakipeleka mahindi kwenye wakala huo au kupitia kwa wanunuzi binafsi.
Kwa
mujibu wa Waziri Tizeba anasema mkulima atauza kuanzia tani moja hadi
mbili na kiwango cha mwisho cha ununuzi kufanywa na NFRA ni tani tano.
Aidha Dkt. Tizeba anasema serikali
imetenga kiasi cha shilingi bilioni kumi kwa ajili ya ununuzi wa
mahindi kutoka kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini.
Mary
Sheto kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anasema Serikali imeweka
mikakati madhubuti kwa ajili ya kuwasaidia wananchi maskini waliopo vijijini ambao asilimia 98 hutegemea kilimo kama njia kuu ya uchumi na maisha yao ya kila siku.
Anasema lengo la Serikali ni kuzalisha tani milioni tano za mahindi ili
nchi ijitosheleze kwa chakula kwa nia ya kupunguza mfumuko wa bei ya
chakula na kuongeza kipato kwa mkulima hatimaye kukuza uchumi na kuuza ziada ndani na nje ya nchi ambako imebainika kuwa na soko kubwa la mazao hayo.
Kwa
mujibu wa Sheto anasema Serikali imefanya mazungumzo na Shirika la
Chakula Duniani (WFP) kwa ajili ya ununuzi wa mahindi hayo na wameonesha
kukubali, lakini kwa masharti ya kuzingatia ubora wa mahindi husika.
“Kwa
kuzingatia hilo, Serikali katika wilaya ambazo zitaanzishiwa utaratibu
huo, wakulima wataelekezwa namna ya kuandaa zao hilo kwa ubora
unaotakiwa kisha kuwahimiza kuwa katika vikundi huko huko vijijini
ambako ununuzi utafanyika” anasema Sheto.
Akifafanua
zaidi Sheto anasema Serikali itahakikisha maghala mapya yanajengwa na
yale ya zamani yataboreshwa kwa kukarabatiwa, ili mahindi yawe katika
mazingira safi kwa lengo la kumvutia mnunuzi atakayenunua zao hilo
katika soko la pamoja la wakulima.
Anaitaja Mikoa itakayofaidika na mpango huo kuwa ni Rukwa /Katavi, Ruvuma, Njombe na Iringa, mikoa ya Kanda ya Ziwa, Dodoma na lingine katika mikoa ya Tanga/Arusha na Kilimanjaro.
0 comments:
Post a Comment