SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Mkoa wa Tanga,
limeishauri serikali kuweka utaratibu maalum utakaowezesha kulipa madai
mbalimbali ya wafanyakazi wa Sekta ya Umma kwa wakati, ili kupunguza
migogoro isiyo ya lazima.
Mwenyekiti TUCTA mkoani hapa, Jacob Barnabas, alsiema hayo juzi mjini hapa na kusema kutokana na ukweli kwamba seikali ndiye mwajiri mkuu nchini, inao wajibu wa kuanza kujenga utamaduni wa kulipa wafanyakazi wake kwa wakati, ili kuepusha lawama zisizo za lazima.
Alisema ili serikali iweze kuonyesha dhahiri kwamba inawajali wafanyakazi wake hivi sasa inapaswa kuanza kulipa kwa wakati madai yao mbalimbali, badala ya kusubiri vitisho vya maandamano na migomo kama ilivyotokea kwa walimu.
Mwenyekiti huyo alisema hatua ya kulipa madai ya wafanyakazi kwa wakati itasaidia kuhamasisha waajiri na wawekezaji wengine kuiga mfumo huo wa serikali ambao utawezesha kujengwa kwa mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na waajiri siku za usoni.
Wakati huohuo, shirikisho hilo limewapongeza walimu nchini waliojitokeza kushiriki katika mgomo uliofanyika Jumatatu wiki hii na kusema hatua hiyo imeonyesha ushujaa na umoja uliopo baina yao.
“Kwa kweli TUCTA Mkoa wa Tanga tumefurahishwa na ujasiri mkubwa ulioonyeshwa na baadhi ya walimu nchini ambao waliondoa hofu na kukubali kusimama mstari wa mbele katika kudai haki zao…licha ya wachache hawakujitokeza kutokana na wasiwasi lakini sisi tunasisitiza kwamba mgomo huo ulikuwa ni halali kwa vile ulifuata taratibu zote za kisheria”, alifafanua Barnabas.
Hata hivyo, TUCTA imewaonya baadhi ya walimu ambao hawakushiriki kikamilifu katika mgomo huo kwa madai ya woga wa kufukuzwa kazi na ubinafsi na kuwataka kuacha mara moja vitendo hivyo kwa kutambua kwamba kupigania haki ni gharama.
Hivi karibuni zaidi ya asilimia 77 ya walimu mkoani hapa walikubali kusaini hati ya kujitokeza kuunga mkono mgomo wa awali uliotarajiwa kufanyika Agosti 15 nchini kabla ya serikali kukimbilia mahakamani kuuzuia
Chanzo;Tanzania
Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment