“Ama kweli hujafa hujaumbika,” walisema
walimwengu wakiwa na maana kubwa kwamba tangu kuzaliwa hadi kufa hupitia
au kukumbwa na mabadiliko mbalimbali, lakini litakavyotokea au lini ni
siri ya Mungu pekee.
Binadamu anaweza kuzaliwa bila kasoro yoyote na
kujijengea matumaini ya kutimiza malengo yake bila wasi wasi, lakini
akapatwa na mkasa utakaofuta ndoto zake zote.
Hivi ndivyo ilivyotokea kwa msichana Zuhura Rajab
mwenye umri wa miaka 17, ambaye kwa mfumo wa maisha ya Kitanzania
hajatimiza ndoto yake hata moja, awe akiishi kijiji au mjini kwani
hajafikisha umri wa kujitegemea.
Mbali na ukweli huo, maisha na ndoto za Zuhura
zimefifia ghafla baada ya kuingizwa na babu yake kwenye imani
iliyogharimu maisha yake na sasa anauguza majeraha kutokana na kuungua
moto huku wataalamu wakisema asilimia 72 ya mwili wake umeathirika kwa
moto.
Mkasa uliomkuta Zuhura hataweza kuusahau maishani
mwake kwani maelezo ya kitaalamu yanaonyesha kuwa akipona, asilimia
chache ya viungo vyake vitaweza kufanya kazi kwa usahihi kwani majeraha
ya moto husababisha ngozi kujikunja.
Ilivyotokea
“Mimi na wanangu tuliitwa nyumbani, tulifika kwa
mganga mimi, mama yangu mzazi pamoja na watoto wangu wawili. Sisi ndiyo
tuliingizwa kwenye shimo, ila baba hakuingia bali alibaki juu na yule
mganga. Hadi tukio linatokea, hakusogea kabisa kwenye lile shimo.”
Ndivyo anavyoanza kusimulia Aziza Hassani (35)
mama wa watoto wawili ambaye yeye na mtoto wake mmoja wamepona kwenye
tukio hilo la moto uliowashwa kwa makusudi na mganga wa kienyeji nao
kuambiwa watoke huku moto ukiwaka na atakayeshindwa, atakuwa amekamatwa
na dawa ya mganga huyo.Anasimulia kwamba November 26 alipigiwa simu na
mama yake mzazi aliyemweleza kuwa kuna dawa (tambiko) la wanafamilia
hivyo yeye na wanawe kutakiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya shughuli
hiyo.
Anaeleza kuwa alifika nyumbani mapema siku hiyo
hiyo akiitika wito wa wazazi wake na kuelezwa kwamba anapaswa kushiriki
kwenye dawa kesho yake Novemba 27, agizo ambalo alikubaliana nalo,
lakini alipouliza ni dawa ya nini alielezwa kuwa ni tambiko.
Aziza anaeleza kuwa walifika kwa mganga huyo na
kuanza kufanyiwa dawa iliyofanyika ndani ya shimo ambalo liliezekwa kwa
nyasi kavu juu yake na kuachwa nafasi ndogo mfano wa mlango, ambao ndiyo
walioutumia kuingilia ndani yake na dawa ilifanyika.
“Mganga alianza kufanya kazi yake sisi tukiwa
ndani ya shimo. Tulikuwa mimi mtoto wangu mdogo Hassan Rajab (4), Zuhura
Rajabu (17) pamoja na mama yangu mzazi, Hadija Abdallah(65) ambaye
ndiye aliyeniita katika dawa hiyo,” anasema Aziza.
Anafafanua kuwa iliwachukua zaidi ya nusu saa
wakiwa ndani ya shimo hilo hadi hatua ya mwisho ya dawa hiyo na
walimwona mganga huyo akiwa amemaliza kufanya mambo yake na kubaki
pembeni ya shimo walilokuwamo.
Baada ya muda walidhani mganga ameshamaliza na kumuuliza
wanaweza kutoka, lakini aliwajibu dawa bado inaendelea na ghafla mganga
huyo aliwasha moto juu ya zile nyasi.
“Moto mkubwa ukaanza kuwaka ndipo mganga
akatuamrisha tutoke shimoni huku moto ukiendelea kuenea hadi mlangoni,”
Aziza anasimulia kwa uchungu.
Anasema kuwa baada ya kauli hiyo ya mganga kuwa
waanze kujiokoa, alianza kumrusha nje mtoto wake mdogo (Hassan) kisha
kuanza harakati za kumsaidia mama yake na mtoto wake mkubwa (Zuhura)
lakini hakufanikiwa kutokana na moto kuwa mkubwa.
“Hivyo mimi niliungua kichwani, mama yangu na mwanangu Zuhura miili yao ikaungua vibaya,” anasimulia.
Anaeleza kuwa baada ya moto kupungua, yule mganga
na baba yake walikuja kuwasaidia kuwatoa ndani ya shimo huku wenzake
wakiwa wameshaungua kiasi cha kushindwa kufanya lolote.
Baada ya kutolewa majeruhi hao baba yake na mganga
walimshauri wasipeleke majeruhi hospitali wakawaeleza kuwa kuna daktari
wao atakwenda kuwatibu katika kijiji cha jirani na hapo walimhakikishia
kuwa majeruhi hao watapona.
Hata hivyo, Aziza anasema kuwa kwa daktari huyo
hakuna kilichofanyika kwa zaidi ya siku tatu na ilipofika Desemba mosi
mama yake alifariki dunia hapo hapo kijijini huku hali ya mtoto wake
ikizidi kuwa mbaya kutokana na kukosa tiba.
“Kwa huyo mganga hakuna tiba waliyopata zaidi ya
kubandikwa pamba kwenye vidonda vyao kwa siku zote tatu. Mama alifariki
dunia kutokana na majeraha yake kuendelea kila siku na maumivu makali,”
anasema Aziza.
Anasema kwamba jambo baya lililokuwa likiendelea
kwa daktari huyo ni vidonda vya majeruhi kuanza kuharibika na kutoa
wadudu hali anayosema ilianza kumtisha zaidi na kuanza kukata tamaa ya
kupona.
Hospitali
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospitali
ya Wilaya Handeni, Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni
Mwanaidi Semboja anasema kuwa walimpokea mgonjwa huyo (Zuhura) akiwa
katika hali mbaya huku vidonda vyake vikiwa havijapata tiba yoyote.
Anasema baada ya kumpokea walianza kumpa tiba za
kitaalamu zaidi ikiwemo kumpunguzia maumivu yaliyotokana na kuungua
sehemu kubwa ya mwili wake hivyo kushindwa kufanya lolote.
“Kwanza tulianza kumpatia dawa za kumpunguzia maumivu kwani
aliletwa akiwa kwenye hali mbaya sana kutokana na kutofungwa vidonda.
Kitaalamu ili kuzuia baridi, tulianza kufanya hivyo na baada ya siku
kadhaa mgonjwa aliendelea vizuri,” anasema.
Muuguzi huyo anasema kuwa kitaalamu binti huyo
ameungua asilimia 72 na kwamba mgonjwa kama huyo anatakiwa kuwa na
uangalizi maalumu kwa muda wote.
Semboja anasema kuwa wanawashukuru wasamaria wema
waliotoa taarifa polisi ambao walifika walipohifadhiwa majeruhi hao,
kisha kuwachukua kuwapeleka hospitali, ambapo yeye Aziza anaendelea
vizuri, huku Zuhura akiendelea kupata tiba na kuhamishiwa Hospitali ya
Mkoa, Bombo mjini Tanga.
Wananchi
Aziza Mkomwa mkazi wa wilayani Handeni anashauri
akisema kuwa ni vyema wananchi wakamrudia Mungu kwa kumwamini na kufanya
ibada misikitini au kanisani, badala ya kuendeleza imani potofu ikiwamo
matambiko.
Anasema ni muhimu kila mtu asimamie kwenye imani
yake ya kidini kwa kufuata yale ambayo vitabu vitakatifu vinamwongoza
badala ya kwenda kinyume na maagizo ya Mungu hata kukutwa na matukio ya
ajabu kama yaliyomkuta Aziza na familia yake.
Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraisser Kashai
anathibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema kuwa mtuhumiwa amekamatwa
na hatua zaidi kuchukuliwa.
captions
Aziza Hassani akimuuguza mtoto wake Zuhura
Rajabu(17) aliyelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni, baada ya
kuungua mwili mzima walipokuwa wakifanyiwa dawa kwa mganga wa kienyeji
ambapo mama huyo alipata majeraha madogo kichwani. Picha na Rajabu
Athumani.
Picha namba 2.
Zuhura Rajabu (17) akiwa amelazwa Hospitali ya
Wilaya ya Handeni akiuguza majeraha ya moto baada ya kuungua alipokuwa
akifanyiwa tambiko yeye na familia yake kwa mganga wa kienyeji wilayani
humo. Picha na Rajabu Athumani.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment