Home » » AJALI YAUA SABA, YAJERUHI 14 TANGA

AJALI YAUA SABA, YAJERUHI 14 TANGA

WATU saba wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kwenda harusini, kuacha njia na kupinduka kwenye Kitongoji cha Kwatondoro, Kijiji cha Magundi, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fresser Kashai, alisema ajali hiyo imetokea Novemba 29 mwaka huu, saa 11jioni.

Alisema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubish Canter, yenye namba T 783 BLM, iliyokuwa ikiendeshwa na Ramadhani Omari (32), mkazi wa Manundu, wilayani humo, ikitokea Kijiji cha Ambangulu, ambayo iliacha njia na kupinduka.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Ali Sengalawa (47), Kihio Rutha, Merina Kitekeko, Asha Musa, Stela Charles (32), Mama Kivula na Jane Mbajo ambao wote ni wakazi wa maeneo mbalimbali wilayani Korogwe.

Waliojeruhiwa ni Ester Akili (58), Amina Mohamed, Zaituni Bakari, Amina Rajabu, Mwaliki Peter (35), Jane Charles, Mariam Sadiki (45), Sai Saliza (42), Mgoshi Bashiri (48), Monica Charles (40) na Veronica Kiondo (43).

Wengine ni Zaina Hamisi (24) na Richard Mosses (18), ambao wameumia sehemu mbalimbali za miili yao na maiti zimehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Magunga kwa utambuzi na uchunguzi zaidi.

"Chanzo cha ajali hakijajulikana, upelelezi bado unaendelea na dereva wa gari anashikiliwa polisi na mmiliki wake kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili," alisema.

Hata hivyo, Kamanda Kashai ametoa onyo kwa madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ongezeko la ajali za barabarani nchini.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa