Home » » WANAFUNZI WA KIKE 800 SEKONDARI KILINDI WAACHA SHULE

WANAFUNZI WA KIKE 800 SEKONDARI KILINDI WAACHA SHULE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Zaidi ya wanafunzi wa kike 800 wa shule za sekondari na msingi Wilaya ya Kilindi, Mkoa wa Tanga, wameacha shule kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baadhi yao kuozeshwa na wengine kuwekwa kinyumba, huku wakiwa na umri mdogo.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa, alisema hali hiyo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kudorora kwa sekta ya elimu wilayani humo.

Alisema hatua hiyo pia inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwa kuwapo kundi kubwa la watu wasio na elimu.

Aliwataka madiwani wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanatumia mamlaka waliyonayo kutunga sheria ndogo ndogo ambazo zitawabana wazazi wa wanafunzi na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Wazazi ndio wahusika namba moja, ambao wanachangia tatizo hili kuongezeka, kwa sababu wanawajua wahusika na hawako tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Lakini pia baadhi yao ndiyo wanaochukua mahari na kuwaozesha watoto wao. Sasa hili ni tatizo na lazima lifanyiwe kazi,” alisema Liwowa.

Akielezea mikakati waliyojiwekea na hatua zitakazochukuliwa, Liwowa alisema kwanza wanataka wawarejeshe watoto kwa wazazi kisha watawakamata wazazi na watuhumiwa waliowakatisha masomo kwa ajili ya kuwachukulia hatua kali za kisheria, zoezi ambalo linaanza utekelezaji wake mapema Agosti Mosi, mwaka huu.

“Katika hili sitakuwa na msamaha na mzazi yoyote atakayebainika kuhusika moja kwa moja na upindishaji wa sheria…yeye ndiye atakuwa mtuhumiwa namba moja. Na naomba waheshimiwa madiwani huko kwenye kata zenu tusaidiane, kwani hili si agizo langu, bali ni agizo la Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara mkoani Tanga mwezi uliopita,” alisema Liwowa.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa