Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Watu watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Kwasunga
wilayani Handeni wamekufa baada ya kula futari ya mihogo inayosadikiwa
kuwa na sumu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema tukio hilo
lilitokea juzi saa 1:00 usiku eneo la Kwasunga Handeni na maiti
zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni.
Kamanda Massawe aliwataja waliokufa kuwa ni Juma
Jumbe (6), Abdi Jumbe (10) na Ramadhani Jumbe (15). Pia alisema kuwa
wazazi wa watoto waliwahishwa hospitali ambako walipatiwa matibabu na
wanaendelea vizuri.
Kamanda Massawe alisema kwa mujibu wa wazazi wa
watoto hao, walikula futari hiyo na baada ya kumaliza, walianza kujihisi
vibaya sambamba na kuishiwa nguvu na alianza kuanguka mmoja baada ya
mwingine.
“Chanzo cha kifo ni futari ya mihogo ambayo kwa
mujibu wa vipimo ilikuwa na sumu. Wazazi wao wako hai ila nao walikuwa
katika hali mbaya, lakini baada ya kupatiwa matibabu wanaendelea
vizuri,” alisema kamanda huyo.
Kamanda huyo aliwataka wote walio katika mfungo
kuichunguza mihogo wanayoinunua kwa ajili ya matumizi ya futari kwani
baadhi haifai kuliwa na binadamu.
“Mhogo unajulikana vyema. Kama mtu ukiumenya na
kuona una rangi za ajabu ajabu ndani, basi achana nao usiupike mingine
haifai kuliwa na binadamu,” alisema Massawe.
Alitoa wito kwa watu kuwa makini.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment