Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tanga, imeahirisha hukumu ya kesi
namba 38/2013 inayomkabili Mweka Hazina wa Manispaa ya Kinondoni, Dar
es Salaam, Alfred Mlowe na wenzake 12 hadi Julai 24, mwaka huu,
kutokana na mmoja wa washitakiwa kushindwa kufika mahakamani.
Kwa sasa Mlowe ni Mweka Hazina wa Manispaa ya Kinondoni, huku
washitakiwa wengine katika kesi hiyo wakiwa wameshastaafu utumishi wa
umma na wengine kuhamishwa katika halmashauri mbalimbali nchini pamoja
na baadhi yao kubaki mkoani Tanga.
Kabla ya kuahirishwa kwa hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Maira Kasonde
alibaini kutokuwapo mahakamani kwa mtuhimiwa, Allen Meena na kumtaka
mdhamini aeleze sababu ya mtuhumiwa huyo kutokuwapo.
Mdhamini wa Meena, alimueleza Hakimu Kasonde kuwa mtuhumiwa huyo
ameshindwa kufika mahakamani kutokana na kusumbuliwa na presha na
malaria.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Kasonde alimtaka mdhamini huyo
kuhakikisha tarehe nyingine itakayopangwa mtuhumiwa anahudhuria
mahakamani.
Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Rickson Lema, Rehema Kajembe,
Lusungu Masangula, Dk. Clement Shembilu, Alfa Moshi, Ally Mkongelwa,
Halima Kaima, Ahmad Shemu, Ramadhani Mzonge na Primi Mamseri.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kati ya Desemba Mosi na 29, mwaka juzi
walitumia madaraka yao vibaya na kumpatia kazi ya ujenzi wa barabara ya
Raskazoni, Mkandarasi Y.N Investment ambaye hakuwa na sifa.
Upande wa mlalamikaji ambao ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) walidai utoaji wa zabuni kwa kampuni hiyo ilikuwa ni
kinyume na kifungu 80(5) cha kanuni ya manunuzi ya umma kutokana na
zabuni kutangazwa mara moja.
Katika habari iliyochapishwa toleo Na 3491 na 3492, ilitafsirika
visivyo, na hivyo kuonekana kama washitakiwa wote ni watumishi wa
Manispaa ya Kinondoni kwa sasa. Tunaomba radhi kwa usumbufu
uliojitokeza.
Chanzo:Tanznia Daima
0 comments:
Post a Comment