Home » » Diwani wa CCM asusia kikao

Diwani wa CCM asusia kikao

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Diwani wa Kata ya Usagara (CCM), Callos Hizza katikati ya wiki hii alitoka nje wakati Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Tanga ukiendelea kama ishara ya kupinga kupitishwa mchoro wa Ramani ya Usagara Mashariki, akidai umelenga kupora eneo la kata yake.
Mchoro huo uliwasilishwa katika mkutano wa baraza hilo na Halmashauri ya Jiji la Tanga, ukitambuliwa kuwa ni wa Usagara Extra namba 2/TA/382/G5.
Hata hivyo, diwani huyo alipinga na kudai wananchi wa kata yake hawakubaliani na njama zinazofanywa kuwapora eneo lao Plot 615 block Z.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mazingira, Danny Mgaza alieleza kwamba mchoro huo umeandaliwa katika eneo la Usagara ikiwa ni marekebisho ya mchoro wa Mipango Miji ya mwaka 1982 ili kufanya uendane kiusahihi na hali halisi ya sasa.
Baada ya kusomwa ajenda hiyo, Diwani Hizza alisema hakubaliani na akafafanua kuwa wataalamu wameupeleka katika mkutano huo ili upitishwe kinyume na utaratibu, kwani ulishapimwa mwaka 2011 kwa ajili maboresho ya eneo la Kata ya Usagara.
Licha ya kutoa ufafanuzi huo, baraza la madiwani liliamua kuupitisha mchoro huo ndipo diwani huyo alipotoka nje kupinga akidai kwamba angeendelea kukaa angekuwa ameshiriki kuwahujumu wananchi wake.
“Wananchi wa Usagara tuna shaka na uhalisia wa kuwasilisha mchoro huu. Tunashuku kwamba eneo lengwa halipo Kata ya Mzingani bali lipo Usagara Kijijini, eneo mkabala na maghorofa ya Bandari na waliomba kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kata au viwanja vya michezo,” alisema Hizza.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa