Wananchi wametakiwa kuwa makini na vocha za pembejeo za kilimo
wanazotumia kwa kuhifadhi vihifadhio vya mbolea hizo ili kudhibiti
wauzaji bandia iwapo mbegu au mbolea walizotumia hazitakuwa na ubora.
Kaimu Ofisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya
Handeni, Yibarila Chiza alitoa tahadhari hiyo juzi alipokuwa akitoa
maelekezo ya kugawa vocha za pembejeo za kilimo kwa wataalamu mbalimbali
wa Tarafa ya Sindeni.
Chiza alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya
kampuni kutoa mbolea za kupandia na mbengu za kukuzia, ambazo hazina
ubora hivyo ni vyema wakulima kuhifadhi vya pembejeo hizo hadi mwisho wa
msimu wa kilimo.
Alisema wamekuwa wakipata malalamiko kutoka kwa
baadhi ya wakulima kuwa, mbolea au mbegu huwa hazina ubora hivyo
kushindwa kupata mavuno ya kutosha kama walivyokusudia.
“Mnatakiwa kuwa makini na mbolea na mbegu bandia,
mtunze vifungashio vya pembejeo hizo hadi mwisho wa msimu wa kilimo,”
alisema Chiza na kuongeza:
“Kama pembejeo hizo zitakuwa na matatizo tuweze
kuwawajibisha wahusika kwani wamekuwa wakiwapatia hasara kwa kutumia
pembejeo zisizo na ubora.”
Pia, aliwataka watendaji wa vijiji, tarafa na kata
kutokuwapa pembejeo hizo wakulima wenye uwezo kwani zimetolewa kwa
ajili wa wakulima wenye kipato cha chini.
Alisema pembejeo hizo ni kwa wale ambao hawajiwezi, lengo likiwa ni kuwasaidia kulima kilimo chenye tija.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment