WAFUGAJI wilayani Kilindi, Tanga, wameitaka serikali kuwatendea
haki sawa na wakulima katika kuchangia ujenzi wa maabara za shule za
sekondari za kata.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, wafugaji hao walisema kitendo cha
serikali kuwatoza sh 3,000 kwa kila ng’ombe mmoja kuchangia ujenzi huo
si sahihi.
Walisema ni vema wakachangia kila kaya kama wanavyochangishwa wakulima.
Magu Kuhanga ni mmoja ya wafugaji wanaoishi Kijiji cha Kilindi,
alisema michango hiyo imekuwa ikitozwa kwa nguvu na baadhi ya watendaji
wa vijiji ambao wanawavizia ng’ombe wanapokwenda kunywa maji.
Alisema wanapofika katika kisima kilichopo katika Kitongoji cha
Saibasi, Kijiji cha Negero, huwakamata wafugaji wasiolipa fedha hizo au
wanalazimka kutoa ng’ombe mmoja kufidia fedha hizo.
Mfugaji Kidagari Mganya, mkazi wa Kijiji cha Mafisa, alisema
serikali kuwatoza wafugaji kwa kichwa kimoja cha ng’ombe kulipa fedha
hizo ni kuwabagua kwa vile wao wanafuga ng’ombe.
“Huu ni ubaguzi kwa sababu wanatuonea sisi wafugaji, wakulima kila
kaya wanachanga sh 10,000 kwanini tusiwe sawa na wenzetu, au kosa letu
ni kuwa na ng’ombe?” alihoji Kidagari.
Alisema mifugo ni kama mazao mengine kwa kuwa inawafanya waishi kwa
kuitegemea na kwamba kama wao wanatozwa fedha hizo kwa ng’ombe mmoja
basi serikali ingewatoza wakulima sh 3,000 kwa kila gunia moja la
mkulima alilopata shambani ili wawe sawa.
Kidagari alisema kutokana na michango hiyo kuwekwa wafugaji
watalazimika kuchangishwa fedha nyingi kutokana na kwamba mtu mmoja
anaweza kumiliki zaidi ya ng’ombe 100.
Mkuu wa Wilaya, Selemani Liwowa, alipoulizwa kuhusu suala hilo
alikiri kuwepo kwa michango hiyo lakini akasema wamepanga kutoza kila
ng’ombe mmoja sh 2,000 na wala si sh 3,000.
“Ni kweli tunawatoza wafugaji sh 2,000 na wala si sh 3,000 waliyosema
na mpango huu tumeubuni kutokana na pato la mtu alilonalo, sasa
tumepanga kila mwenye ng’ombe atalipa sh 2,000 kwa ng’ombe mmoja,
kondoo na mbuzi mmiliki wake atalazimika kulipa sh 500 kwa mnyama
mmoja,” alisema Liwowa.
Mkuu huyo wa wilaya alisema michango hiyo wameiweka kulingana na
kipato cha mtu, akatoa mfano kuwa yeye kama mkuu wa wilaya amelazimika
kuchangia ujenzi huo kwa kutoa sh 500,000 kutoka katika mshahara wake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment