Lushoto. Wakulima wa Kilimo
cha Mbogamboga na Matunda wilayani Lushoto, mkoani Tanga, wameomba
Serikali kuwapunguzia gharama za pembejeo za kilimo ili walime kisasa.
Wakizungumza kwenye kikao cha Umoja wa Wakulima
wa Mbogamboga na Matunda Wilaya ya Lushoto na Korogwe ulioitishwa na
Shirika la Oxfam Tanzania tawi la Lushoto juzi, wakulima hao walisema
kwa kipindi kirefu wameomba Serikali kupunguza gharama bila ya
mafanikio.
Walisema hali hiyo imekuwa ikirudisha nyuma
jitihada zao, badala yake kulima kwa mazoea jambo ambalo linawafanya
wengi kutokuona faida ya kilimo.
“Tumekuwa tukikutana na kutoa kero zetu bila
kupatiwa ufumbuzi, hutujui tuwasilishe vipi ili Serikali itusikilize...
tumekuwa tukipoteza muda wetu kila siku,” alisema Juma Dhahabu na
kuongeza:
“Oxfam kwa upande wenu tunawashukuru kwa kutupatia
msaada mdogomdogo na kutukutanisha na wataalamu wa kilimo na wadau
wake.” Dhahabu alisema ni jambo la kushangaza kuona mkulima wa Lushoto
akiwa maskini ilhali wilaya hiyo ina rutuba inayofaa kwa aina tofauti
za kilimo, ikiwamo kilimo cha njegere, hivyo kuitaka Serikali kuwaunga
mkono hasa pembejeo
Naye Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Lushoto,
Jumanne Shauri alitaka Oxfam kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha
mbogamboga na matunda, kwa sababu wengi hawana elimu hiyo.
Shauri alisema baadhi ya wakulima hawana elimu
hivyo kushindwa kulima kilimo chenye tija. Alisema iwapo mkulima wa
njegere atapatiwa elimu stahiki, ni wazi wakazi wengi wa Lushoto na
Korogwe watakimbilia kilimo hicho.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment