WAZEE wanaoishi kwenye kambi ya ukoma iliyopo Ngomeni, wilayani
hapa, wameiomba serikali kuwajengea uzio ili kuwanusuru na vibaka
wanaowavamia mara kwa mara na kupora mali zao, ikiwemo mifugo.
Walitoa ombi hilo wakati wakipokea msaada wa nguo na chakula kutoka
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga
wakati ilipotembelea kambi hiyo.
Walisema kambi hiyo ipo mbali na makazi ya watu, hivyo inakuwa rahisi
kwa vibaka na wezi kuwavamia mara kwa mara, hasa katika kipindi
wanachopelekewa misaada.
“Tunaiomba serikali ituangalie katika suala la kujengewa uzio na
uhakika wa majisafi na salama, kwani kwa sasa hakuna, inatulazimu
kwenda mwendo mrefu kutafuta maji. Bwawa lililochimbwa kwa ajili yetu
limekauka,” alisema Mohamed Salimu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mathew Mganga, alisema kambi
hiyo ina wazee 86 ambao wanatumia matundu matatu ya vyoo ambayo
hayalingani na idadi yao.
Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Edson Makallo, alisema iwapo
watendaji kwenye ngazi zote wangeweza kusimamia fedha za maendeleo na
kuhakikisha zinawafikia walengwa, rushwa nchini ingepungua au kwisha
kabisa
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment