MASHABIKI wa soka mkoani Tanga, wameliomba Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kutoa elimu kuhusiana na mfumo mpya wa tiketi
unaotolewa kwa njia ya kieletroniki kwani umewaleta adha.
Wakizungumza jijini hapa juzi, walisema kuwa hawapingi kuwepo na
mfumo huo, bali hakukuwa na maandalizi kwa kutoa elimu kwa mashabiki,
hivyo wanaona kama shirikisho hilo limekurupuka na kushauri bora
ungeanza mwakani na muda huu wautumie kuelimisha kuhusiana na matumizi
ya mfumo huo.
Mmoja wa mashabiki hao, Athumani Mnyamisi, alisema kuwa shirikisho
hilo limekurupuka, hivyo ni bora wangeacha hadi mwakani, hivyo kipindi
hiki wakitumie kuelimisha wadau au mashabiki wa soka ili waweze kuwa na
uelewa utakaofanya kusitokee mgogoro.
“Mfumo huu mi naona kama wamekurupuka, kwa sababu sisi mashabiki
hatuna uelewa na hili jambo, kwani tumefika uwanjani toka saa nane
milango ni miwili tu inatumika, mpaka saa kumi na nusu mpira umeanza
bado hatujaingia uwanjani,” alisema.
Shabiki mwingine, Salimu Abdallah, aliupongeza mfumo huo kuwa
unapunguza ubadhirifu wa fedha ila bado mashabiki wengi wa soka hawana
uelewa nao, hivyo itachukua muda kuweza kufahamika na kutumika bila
vikwazo hapa nchini.
Hata hivyo, Meneja wa Uwanja wa Mkwakwani, Mbwana Msumari, alisema
kuwa tatizo mashabiki wa soka hawana uelewa na mfumo huo, hivyo
kulazimika kutumia mfumo wa zamani wa kuuza tiketi kwa kawaida.
“Nimenusurika kupigwa na mashabiki kutokana na kushindwa kuuelewa
mfumo huu na bei ya tiketi kupanda, badala ya elfu tatu kwa mechi
imekuwa elfu tano, hivyo tukalazimika kuuza tiketi kwa mfumo wa zamani
ili mashabiki waweze kuingia na kutazama mpira,” alisema Msumari.
Katika mechi hiyo, wenyeji Coastal Union walipata bao dakika ya
kwanza likifungwa na Yayo Lutumba huku JKT Oljoro kutoka Arusha
wakisawazisha dakika ya 87 kwa bao la Amisi Salehe.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment