JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu watano kwa tuhuma
za kukutwa na bunduki aina ya Shotgun na sare za Jeshi la Polisi
ambazo zilitumika katika matukio ya uhalifu wilayani Korogwe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alisema jana
kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 28 mwaka jana, saa 4 usiku
katika eneo la Kambi ya Mkonge ya Gomba, Kata ya Makuyuni, Tarafa ya
Mombo.
Alisema watuhumiwa hao walikuwa wakiitumia bunduki hiyo yenye namba
za usajili 807028 ikiwa na risasi tatu na ganda moja katika kufanyia
uhalifu katika maeneo mbalimbali.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Zakaria Jelas (50), Moses Jonas
(44), Selemani Hassan (21), Taratibu Hemed (74) na Hemed Taratibu (32),
wote wakazi wa Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro.
Kamanda Massawe alisema baada ya upekuzi watuhumiwa hao walikamatwa
na sare mbili mali ya Jeshi la Polisi Tanzania zikiwemo shati mbili za
polisi na suruali ambayo waliikata kama kaptula na kwamba walipohojiwa
walikiri kuhusika na matukio mbalimbali ya unyang’anyi na utekaji wa
magari.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani Tanga linawashikilia
wakazi watatu kwa tuhuma za kupatikana na mali inayodhaniwa kuwa ni
ya wizi.
Watu hao walikamatwa juzi, saa 6 mchana katika kizuizi cha Polisi
kilichopo Kijiji Kwasunga, Kata ya Makuyuni, Tarafa ya Mombo, wilayani
Korogwe wakiwa na pikipiki mbili za wizi ambazo ziliibiwa Kariakoo, Dar
es Salaam.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Jackson Aloyce (25) na Leonard
Frederick (21) wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili T 274 CQV
Boxer rangi ya bluu na Karist Adolf (22) akiwa na pikipiki T 162 CKL
Boxer, rangi nyeusi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment