Home » » LAAC yaagiza mwanasheria aonywe

LAAC yaagiza mwanasheria aonywe

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)
Kamati ya Bunge ya Hesabu za  Serikali za Mitaa (LAAC) imeagiza aliyekuwa Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga apewe onyo kali kwa kushindwa kuitetea mahakamani na kusababisha wafanyakazi kushinda kesi.
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wake, Rajabu Mbarok kwenye ziara ya wajumbe wa kamati hiyo iliyofanyika wilayani hapa ambayo iliambatana na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.

 Alisema Mwanasheria huyo ambaye kwa sasa amehamishiwa katika halmashauri nyingine ya wilaya iliyopo mkoani humo anastahili kupewa onyo kali kwa kitendo chake cha kuifanya halmashauri ya Muheza kushindwa katika kesi hiyo dhidi ya wafanyakazi wake.

Alisema kitendo cha mwanasheria huyo kushindwa  kuitetea halmashauri hiyo mahakamani kimewapa ushindi wafanyakazi hao na kurudishwa kazini.

 Awali akitoa taarifa mbele ya kamati hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu alisema kwa halmashauri ya wilaya hiyo imepata hati safi  kwa miaka mitano mfululizo  katika hesabu za serikali.

Alisema halmashauri hiyo imekuwa ikipata hati safi za mahesabu kila wakikaguliwa na mkaguzi wa mahesabu wa nje.

Alisema kutokana na uaminifu wa kutumia fedha za serikali vizuri  katika miradi, wataendelea kupata hati safi kila mwaka.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbarok alipongeza jitihada zao hizo na kuwataka kutumia fedha zinazoletwa na serikali kwa miradi iliyokusudiwa ili wananchi wapate maendeleo.

Naye Mwakilishi wa Ukaguzi wa Mahesabu ya Serikali (CAG)  wa Nje  aliyejitambulisha kwa jina moja la Christopha, alisema kuwa wamepokea taarifa za mahesabu kutoka halmashauri hiyo lakini bado taarifa nyingine hazijakamilika.
CHANZO: NIPASHE



0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa