Home » » Wajenga kituo cha polisi kukabili kilimo cha bangi

Wajenga kituo cha polisi kukabili kilimo cha bangi

WANANCHI wa Tarafa ya Magoma wilayani Korogwe, wakishirikiani na Mbunge wao Steven Ngonyani wameamua kujenga kituo cha polisi kudhibiti kilimo cha bangi na ujambazi. Mbunge Ngonyani aliyaeleza hayo kwenye harambee ya uchangishwaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

“Panapostahili kuleta maendeleo ya haraka kutokana na tatizo ambalo linalotukabili basi wananchi tushirikiane kutatua na siyo kusubiri serikali,” alisema.

Alisema ujenzi wa kituo hicho utaimarisha ulinzi na usalama kwenye tarafa hiyo na kudhibiti kwa kiasi kikubwa kilimo cha bangi.

Kilimo cha bangi katia tarafa hiyo kimekuwa ni tatizo kubwa licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na polisi ikiwamo kuchoma mashamba hayo, alisema.

“Tarafa hii inaongoza kwa kilimo cha bangi hivyo wananchi tushirikiane kuhakikisha tunachangishana kwa hali na mali kuhakikisha kituo hiki kinakamilika kwa wakati i kupiga vita kilimo hicho cha bangi,” alisema 

Aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Korogwe Vijijini kuacha tabia ya kutegemea serikali kuu pekee kuwaletea maendeleo.

Mbunge huyo alisema wakati mwingine fedha kutoka serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo haziji kwa wakati.

“Wilaya ilikuwa inakufa kwa kutegemea fedha kutoka serikali kuu lakini kumbe wananchi wakihamasishwa wanaweza kuleta mabadiliko mengi hivyo tumeamua kuishirikisha serikali ya wilaya kwa ajili ya kuharakisha maendeleo kwenye sekta mbalimbali wilayani hapa,”alisema 

Naye Diwani wa Kata hiyo, Hadija Mshahara alisema ujenzi wa kituo hicho si kwa ajili ya kukamata wananchi bali ni kwa ajili ya usalama wa kata kutokana na kuwa mbali na huduma hiyo kwa sasa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa