Home » » Wanawake wapewa somo la ujasiriamali

Wanawake wapewa somo la ujasiriamali



na Elizabeth Kilindi, Tanga

WANAWAKE wajasiriamali kupitia vikundi vyao wameaswa kutumia mikopo wanayopewa kwa makini ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kukumbuka kwamba mikopo wanayopewa na mfuko si sadaka bali inapaswa kurejeshwa kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Mzamili Shemdoe, wakati akifungua mafunzo ya siku nne ya biashara kwa vikundi vya wanawake vitakavyopata mkopo wa awamu ya 24, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF).
Pamoja na mambo mengine Shemdoe aliwataka wanawake hao kuwa watulivu kwa kipindi chote cha mafunzo ili kuweza kufaidika na mada zitakazofundishwa na hatimaye kuweza kuwaletea tija katika biashara zao.
Alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imekusudia kutoa mkopo wenye thamani ya sh milioni 35.
Aidha, alisema hadi sasa jumla ya wanawake 5,445 kutoka vikundi 1,089 wameshahudimiwa na mfuko huo.
Sambamba na hilo ameitaka almashauri kuendelea na juhudi zake za kuvikopesha vikundi vya wanawake na kuhakikisha wanakuwa na maisha bora.
Shemdoe alisema Idara ya Maendelleo ya Jamii itatumia kanuni na taratibu zinazosimamia mfuko kuvibana vikundi visivyorejesha kwa wakati na kuvifikisha katika mabaraza ya kata na hatimaye mahakamani ili kuongeza kasi ya marejesho na wanawake wengine waweze kunufaika na mfuko huu.
“Naamini kabisa kama wadau wa mfuko huu mtaweza kuhamasishana na kurejesha kwa wakati ili kuweza kutoa mikopo kwa kasi kubwa zaidi ya kupita ilivyo sasa,” alisema Shemdoe.
Alitumia fursa hiyo kuwaagiza maofisa maendeleo ya jamii kuwaelekeza wanawake kwenye asasi za fedha zinazotoa mikopo yenye masharti nafuu ili kupata huduma kama zinazotolewa na mfuko huo.
Pia aliwataka wanawake kujiunga katika vyama vya akiba vya kuweka na kukopa (SACCOS) zilizoko kwenye kata kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupunguza mrundikano wa maombi ya vikundi vinavyosubiri uwekezaji kupitia mfuko huu ambao kwa sasa uwezo wake ni mdogo.

CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA 

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa