na Mohammed Mhina, Handeni
MAHAKAMA ya Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga,
imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi wa Kijiji cha Kibirashi, Ramadhani
Samselo (20) baada ya kupatikana na hatia ya kupora pikikipiki (bodaboda) kwa
kutumia silaha.
Akitoa hukumu hiyo jana mbele ya umati uliokuwa
umefurika mahakamani hapo wakiwamo waendesha bodaboda wa wilaya za Kilindi na
Handeni, Hakimu Maligana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Patrick
Maligana, alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka,
hivyo kumtia hatiani mtuhumiwa bila shaka kwa kosa aliloshitakiwa nalo.
Alisema anatoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa
wengine wanaowania mali za watu wengine wakati wakitafuta kipato halali.
Alipotakiwa kujitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu
hiyo, mshitakiwa alieleza kuwa anaiachia mahakama itoe adhabu inayomfaa.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Nzagalila
Kikwelele, alidai Januari 29 mwaka huu, majira ya saa 2:00 usiku mwaka huu huko
Kibirashi, Samselo akijifanya ni msafiri na kukodi pikipiki (bodaboda) ya
Mngoya Kigono, ili impeleke nyumbani kwake.
Alidai wakiwa njiani mtuhumiwa Samselo alianza
kumshambulia mwendesha bodaboda huyo kwa kisu sehemu ya mbavuni na mikononi na
baadaye kuanguka chini na kumpora pikipiki hiyo T. 959 AXN Sunlag.
Alidai baada ya mtuhumiwa kuondoka eneo la tukio,
mlalamikaji alimpigia simu mmoja wa waendesha bodaboda mwenzake na ndipo
walitoka kwa wingi kumfuatilia na kumkuta akiwa amelala chini huku akitokwa na
damu nyingi ambapo walimchukua kumpeleka hospitalini huku wengine wakimfuatilia
mtuhumiwa.
Alidai vijana hao walipofika mbele kidogo walimkuta
mtuhumiwa akiongeza mafuta lakini alitimua mbio na kuiacha pikipiki hiyo baada
ya kubaini alikuwa akifuatiliwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment