Home » » Mwakyembe azuia anasa kwenye ndege

Mwakyembe azuia anasa kwenye ndege



na Bertha Mwambela, Tanga
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amepiga marufuku wafanyakazi wa wizara yake kusafiri kwa ndege katika daraja la kwanza wanapokwenda nje ya nchi, akidai huo ni uharibifu wa fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Dk. Mwakyembe alisema kuanzia sasa wafanyakazi wote wa serikali walioko chini ya wizara yake ni marufuku kusafiri kwa ndege wakitumia daraja la kwanza na kuonya kuwa atakayebainika fedha yake itakatwa kwenye malipo yake.
Alisema anayetakiwa kusafiri na ndege daraja la kwanza ni rais pekee na si watendaji wengine, jambo alilodai kuwa hata kwenye nchi nyingine wanawashangaa kwa utaratibu wanaoutumia wa kuharibu fedha zinatokana na kodi za wananchi.
“Inanishangaza sana kuona baadhi ya watendaji hawana uchungu na fedha za Watanzania, sasa nasema marufuku kuanzia leo kwa wafanyakazi wote walioko chini ya Wizara ya Uchukuzi, kusafiri kwa ndege daraja la kwanza, naomba wote tutumie daraja la pili,” alisema Waziri Mwakyembe.
Alisema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanajipanga ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimepangwa kuboreshwa na kila mtu kuwajibika katika nafasi yake ili kuweza kufikia malengo ya kuboresha sekta hiyo.
Waziri Mwakyembe aliongeza kuwa, hatakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote ambae hataweza kufikia malengo ya utendaji kazi waliojipangia kama wizara, ili kukabiliana na ushindani wa nchi jirani za Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alisema anao uhakika wa kusonga mbele kwa bandari ya Tanzania kwani bodi ya wakurugenzi aliyoiteua hivi karibuni ana imani nayo.

CHANZO HABARI LEO

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa