Home » » WAFUGAJI WAGOMA KUONDOKA

WAFUGAJI WAGOMA KUONDOKA



na Efracia Massawe, Kilindi
WAFUGAJI wa kata ya Msanja, wilaya ya Kilindi, mkoani Tanga, wamesema licha ya serikali kuwapa siku 14 kuondoka katika eneo hilo, hawako tayari kufanya hivyo mpaka watakapopatiwa eneo mbadala la kufuga mifugo yao.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa niaba ya wafugaji wenzake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Luis Qorro, alisema mgogoro unaoendelea katika eneo hilo, umesababishwa na viongozi wa serikali za mtaa kuwadhibiti wakulima na wafugaji.
Alisema wengi wa wafugaji na wakulima katika eneo linaloleta mgogoro, waliingia miaka sita iliyopita baada ya serikali kutoa tamko la kugawa maeneo hayo kutumika rasmi kwa ajili ya wanakijiji wakiwemo wafugaji.
“Tumeshtushwa na agizo la mbunge wa eneo letu kutupa siku 14, huku akitoa kauli kuwa yuko tayari kuuza kitu chake cha thamani ili kuishinikiza serikali ituondoe hapa. Kwa sababu hiyo tunahisi serikali inatunyanyasa maana haikumbuki tamko lake la awali,” alisema Qorro.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), alikanusha madai hayo na kusema hajafika eneo hilo takriban miezi mitano sasa, ila kuna uwezekano wa mkuu wa wilaya hiyo kutoa agizo hilo kutokana na wengi wao kuvamia eneo hilo kinyemela.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa