Home » » KIZIMBANI KWA KUGOMA KULIPA USHURU

KIZIMBANI KWA KUGOMA KULIPA USHURU



Na Amina Omari, Muheza
WAFANYABIASHARA saba wa Kijiji cha Mkanyageni Kata ya Ngomeni wilayani Muheza, wamefikishwa mahakamani, kwa kosa la kugoma kutoa ushuru wa Sh 1000.

Wafanyabiashara hao walifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo jana na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Ally Kondo, ambapo walisomewa shitaka mbele ya Hakimu, Jeni Kivambe.

Wafanyabiashara waliofikishwa mahakamani hapo ni George Kihiyo, Abedi Issa, Martin Samweli, Ismail Yahaya, Lizi Kasembe, Salehe Cheta na Juma Hamadi, wote wakazi wa Kijiji cha Mkanyageni.

Hakimu Kivambe alisema, wafanyabiashara hao wanakabiliwa na kosa la kugoma kulipa ushuru wa mwezi, kutokana na kuwa risiti hazina nembo ya halmashauri ya wilaya.

Hakimu huyo alisema, wafanyabiashara hao pia wanakabiliwa na shitaka la kumgomea mtendaji huyo wa kijiji, kutoa fedha hadi waonyeshwe risiti halali za Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.

Washitakiwa hao walikana shitaka hilo na kwamba kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 18 mwaka huu.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa