Home » » MBUNGE CUF AWATAKA WANANCHI KUIWAJIBISHA SERIKALI

MBUNGE CUF AWATAKA WANANCHI KUIWAJIBISHA SERIKALI

Na Bakari Kimwanga, Muheza
MBUNGE wa Viti Maalumu (CUF), Amina Mwidau, amesema ili Taifa liweze kupiga hatua kimaendeleo, ni lazima wananchi wakubali kuiwajibisha Serikali kuanzia ngazi za vijiji.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, alipohutubia mkutano wa ndani ya CUF Wilaya ya Muheza na kuwataka viongozi wa chama hicho kuhakikisha wanajenga na kukiimarisha kwa kutoa elimu ya utambuzi wa wananchi.

Alisema usimamizi mbovu kwa watendaji wa Serikali unataokana na sera mbovu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoahidi maisha bora kwa kila Mtanzania katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza, lakini hadi sasa hakuna kilichotekelezeka.

“Kwa kipindi cha miaka mitano ya awali ya Rais Kikwete kila Mtanzania alikuwa na hamu ya kuona anapata maisha bora kama ilivyoahidi Serikali ya CCM, nasi kama wabunge wa upinzani tumekuwa tukiwasuta na hata kutaka kuona utekelezaji wake ndani ya Bunge, ila ni wazi wameshindwa.

“Sasa umefika wakati kwa viongozi wa chama chetu kuanzia ngazi ya matawi hadi wilaya kuanza kutoa elimu kwa wananchi namna bora ya kuiwajibisha Serikali ya CCM. Wananchi wanatakiwa kuhoji sera na mikakati, ikiwamo mapato na matumizi ya Serikali za Vijiji vyetu pamoja na ngazi ya wilaya.

“Ninajua Muheza ina changamoto nyingi, hasa kwa wananchi kukosa huduma muhimu za kijamii, ikiwamo elimu, afya na hata ubovu wa miundombinu, hasa katika barabara zetu za kuelekea maeneo ya vijijini,” alisema Mwidau.

Katika mkutano huo, aliwapokea wanachama wapya kutoka vyama vya CCM na CHADEMA, huku aliyewahi kuwa kada wa CCM, Hamis Rajab maarufu kwa jina la Mgosi, naye alitangaza kujiunga na CUF.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi ya uanachama, Mgosi, alisema amerudi ndani ya chama cha wanyonge ambacho ni kimbilio la Watanzania wote.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa