Home » » DC AWATAKA WATENDAJI KUACHA UBINAFSI

DC AWATAKA WATENDAJI KUACHA UBINAFSI

Na Amina Omari, Tanga
MKUU wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, amewaagiza watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi na kuacha ubinafsi.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha Baraza la Ushauri la Wilaya (RCC), Dendego alisema halmashauri hiyo ni mali ya wananchi, hivyo ni wajibu kwa watendaji hao kufanya kazi kwa maslahi ya umma.

“Tusifanye kazi kwa mazoea, kusukumwa au kwa ubinafsi, tupo hapa kwa ajili ya kuwatumikia wakazi wa Tanga ili kusimamia harakati za maendeleo, hivyo tusiwe sababu ya kurudisha nyuma maendeleo hayo,” alisema Dendego.

Pia aliwaagiza kuacha visingizio visivyo na sababu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, kwani vitu hivyo ndio vinavyochangia ufanisi duni wa kazi na malalamiko kutoka kwa wananchi.

Alisema nafasi ipo wazi kwa mtendaji anayeona hawezi kuchapa kazi kwa ufanisi na kwa wakati kuhama katika halmashauri hiyo kabla hatua za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yake.

Alisema Tanga ya sasa inahitaji watendaji ambao watafanya kazi kwa ubunifu bila ya kusukumwa na kwa malengo waliyojiwekea ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sasa.

Hivyo aliwaagiza wakuu wa idara, wenyeviti wa mitaa, kata na tarafa kuandaa mpango kazi wa maendeleo katika sehemu zao na kuwasilisha kwake ndani ya siku saba, ili kubaini changamoto pamoja na malengo waliyojiwekea.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa