Na Amina Omari, Tanga
HATIMAYE Serikali ya Kata ya Kichangani, mkoani Tanga, imejimilikisha viwanja 560 ambavyo awali vilikuwa vinashikiliwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya watu.
Kauli hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kata hiyo, Rajab Ramadhani, katika mkutano mkuu wa kata hiyo, wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Mgogoro wa Ardhi iliyoundwa kutafuta ufumbuzi wa viwanja hivyo.
Alisema katika kupitia upya mipaka ya kata hiyo, wamebaini Halmashauri ya Tanga imeingilia mipaka ya kata hiyo na kuanza kupima viwanja katika eneo hilo la Kange bila kuishirikisha Serikali ya Kata, jambo ambalo limesababisha migogoro ya ardhi katika sehemu hiyo.
“Baada ya kufanya upembuzi yakinifu tumeona kuwa Jiji walivamia eneo lile na kujimilikisha viwanja isivyo halali, hivyo kwa sasa tumechukua viwanja vyetu na tunaandaa utaratibu mpya wa ugawaji ambao utazingatia haki kwa wananchi,” alisema Ramadhani.
Alisema kutokana na jiji kuvunja sheria kwa kuchukua ardhi ya kijiji bila idhini, wameamua kuichukua ardhi hiyo na viwanja hivyo vitagawiwa kwa wanakiji hao.
Hata hivyo, Mtendaji wa Kijiji hicho, Abdalah Shaitwa, alisema wataanza mchakato wa kugawa viwanja hivyo pamoja na kugawa hati za kumiliki eneo kwa ajili ya kuepuka kuchukuliwa kama hapo awali.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment