na Mbaruku Yusuph, Tanga
KATA ya Ngamiani Kusini jijini Tanga inatarajiwa kutumia sh milioni 114 katika ujenzi wa barabara ya Mauwa yenye urefu wa kilometa 0.5 kwa kiwango cha lami.
Akizungumza na Tanzania Daima, Diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni Naibu Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Tanga, Mussa Mbaruku alisema utekelezaji wa mradi huo na miradi mingine ya ujenzi wa barabara itakayokuwa endelevu katika kata hiyo, ni kutokana na ushirikiano mzuri wa Halmashauri ya Jiji.
Mbaruku alisema kata imepokea sh milioni 114 kutoka Serikali Kuu na Halmashauri ya Jiji kwa kushirikiana na Mfuko wa Barabara.
Aidha alisema changamoto zinazokabili utekelezaji na uboreshaji wa miundombinu katika kata yake, ni serikali kutenga bajeti ndogo ya miradi ya maendeleo katika halmashauri, kutokukamilika kwa bajeti hiyo na kutolewa kwa awamu kitu kinachosababisha kukwamisha malengo ya maendeleo ya kata zote zilizopo katika Halmashauri ya Jiji.
Alisema ipo haja sasa kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga kuongeza bajeti na kuona haja ya kufanya mtandao wa kuunganisha barabara zenye kiwango cha lami kwa jiji zima na kuondoa kero ya ubovu wa barabara iliyopo.
Hata hivyo, aliwaomba madiwani wenzake kuhudhuria vikao vya mitaa ili kujua kero za wananchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo kwa kuzingatia kwamba ndio waliowaweka madarakani hayo hivyo ni wajibu wao kuwatumikia.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment