Home » » KOROGWE YARIDHIA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME

KOROGWE YARIDHIA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME


Na Oscar Assenga, Korogwe
HALMASHAURI ya Wilaya ya Korogwe imeridhia utekelezwaji wa mradi wa kuzalisha umeme unaotokana na nguvu za upepo, utakaoendeshwa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Redcot na wafadhili kutoka Sweden.

Maridhiano hayo yamefikiwa hivi karibuni katika kikao cha madiwani, huku upembuzi yakinifu ukiwa umefanywa kwa msaada wa Serikali ya Denmark kupitia DANIDA, ambapo mkurugenzi mtendaji wa Redcot, Julius Kilimoya alitoa tarifa ya mradi huo kwa wajumbe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Redcot, aliwaeleza wajumbe wa Baraza la Madiwani kuwa iwapo mradi huo utatekelezwa utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Korogwe, kwa kuwa na uhakika wa kutumia umeme watakuwa wakiuzalisha wenyewe.

Alisema iwapo mradi huo utakamilika wamiliki wake watakuwa Kampuni ya Redcot, Serikali ya Kijiji cha Goha na wafadhili kutoka Sweden.

Alisema umeme utakaozalishwa utatoa megawati 50.

Alisema umeme huo utatosheleza matumizi ya Wilaya ya Korogwe ambayo matumizi yake si zaidi ya megawati mbili, huku ziada inaweza kuuzwa hata katika Gridi ya Taifa.

“Nimekuja hapa kuwapatia taarifa za mradi huo na kuomba ridhaa yenu kuuendesha ili mtupatie eneo, mradi huu ukikamilika utaongeza umeme kwa matumizi ya wilaya ambapo bei itakuwa nafuu na nyongeza inaweza kuuzwa kwenye Gridi ya Taifa,” alisema Kilimo.

Alisema nchi mbalimbali duniani zimeweza kunufaika na matumizi ya umeme huo utokanao na nguvu za upepo.

Alisema ili mradi huo ukamilike, wameomba kupatiwa eneo lenye ukubwa wa ekari 200 katika Kijiji cha Goha, ambapo wataweza kufunga mashine, kujenga karakana na chuo cha teknolojia huku wakifikiria kufanyika kwa upanuzi siku zijazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Korogwe, Sadick Kallaghe, alimtaka mkurugenzi huyo kuwasiliana na mkurugenzi wa halmashauri kwa ajili ya kuendelea kujadili mchakato wa uzalishaji umeme huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa