Home » » CHADEMA TANGA YALAANI MAUAJI MORO

CHADEMA TANGA YALAANI MAUAJI MORO



na Mbaruku Yusuph, Tanga
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Tanga kimelaani vikali vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Polisi nchini vya kuzuia maandamano na mikutano inayofanywa na chama hicho na kusababisha hasara kubwa ikiwemo kupoteza maisha ya wanachama.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, Benson Mramba, alisema vitendo vinavyofanywa na jeshi hilo ni kuingilia demokrasia na kuvuruga uhuru wa vyama vingi nchini.
Alisema ni lazima jeshi hilo litoe uhuru kwa vyama vya upinzani, ili kuweza kukuza demokrasia na kutoa nafasi kwa vyama hivyo viweze kueleza sera zake kwa wananchi na si kuzuia kama wafanyavyo sasa.
“Jeshi la Polisi limekuwa na tabia kila wakati kuingilia maandamano au mikutano ya chama hicho na kusababisha mauaji kama hayo ambayo yalitokea mkoani Morogoro na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa wala tume ya uchunguzi kuundwa juu ya mauaji hayo kwa raia asiyekuwa na hatia,” alisema.
Hata hivyo, alisema chama hicho kilijiandaa vema kupokea mwili wa marehemu, Ally Zona aliyeuawa wakati wa maandamano ya Operesheni Sangara yaliyofanyika mkoani Morogoro na hatimaye kushirikiana na ndugu wa marehemu huyo katika mazishi yaliyofanyika nyumbani kwao Kijiji cha Sengano kata ya Kilulu wilayani Muheza mkoani hapa.
Katibu alisema wakati wa maandalizi ya mazishi ya kijana huyo kulijitokeza mambo mbalimbali, ikiwamo suala la udini, ukanda na ukabila, hali ambayo ilileta picha mbaya na kusema kuwa mambo hayo ni uchochezi na masuala ambayo yanatengenezwa kwa masilahi ya watu binafsi kwa ajili ya kukichafua chama hicho.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa