Home » » DC MUHEZA AKAMATA MBAO ZILIZOVUNWA KWA MAKOSA

DC MUHEZA AKAMATA MBAO ZILIZOVUNWA KWA MAKOSA

Na Amina Omari, Muheza
MKUU wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, amezikamata mbao haramu zaidi ya 173, zinazotokana na miti ya miembe, huku akiwataka viongozi wa Serikali za Vijiji kurudisha ardhi iliyouzwa holela.

Mbao hizo zilikamatwa juzi katika Kijiji cha Mtiti, Kata ya Kigombe wilayani Muheza alipofanya ziara ya kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi na Katiba katika Vijiji vya Kigombe na Msakangoto.

Hatua hiyo ya kukamata mbao hizo imekuja baada ya wananchi wa kijiji hicho kufichua ukataji miti huo kinyume na sheria katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika Shule ya Msingi Mtiti.

Mkazi wa Mtiti, Athumani Shabani, alimweleza DC huyo kuwa, sasa miti ya miembe inakwisha kwa kukatwa na kupasuliwa mbao na watu huku viongozi wa kijiji hicho akiwamo mwenyekiti wa kijiji, ofisa mtendaji wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji kutochukuwa hatua zozote dhidi ya uharibifu huo.

“Kama ninayosema huamini basi nakuomba mkuu tutoke wote mguu kwa mguu twende sehemu ambazo miembe hiyo imekatwa ukaone jinsi uharibifu uliofanywa na viongozi wa Serikali kushindwa kuchukuwa hatua zozote na taarifa wanazo,” alisema Shabani.

DC huyo alikubali kwenda sehemu ya tukio ambapo alijionea miti ya miembe imekatwa na kukuta mbao zaidi ya 173 zimerundikwa zinangojea kusafirishwa.

Baada ya kuona hivyo, alimuagiza Diwani wa Kata ya Kigombe, Kombo Juma na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kigombe, Mohamed Kitabu, kuzichukuwa mbao hizo na kudhihifadhi katika Shule ya Msingi Kigombe kwa ajili ya kupanga matumizi ya mbao hizo na mhusika aliyepasua mbao hizo, Luka Marasta, anasakwa baada ya kutoroka.

Alisema ni marufuku kuvuna miti yoyote ama kusafirisha mbao, kwa kuwa amepata taarifa watu wanakata miti ya matunda na wanaharibu mazingira na kuuza ardhi ya kijiji zaidi ya heka 100.

Katika hatua nyingine, wananchi hao walimweleza kuwa ardhi ya kijiji hicho inauzwa kama karanga na viongozi wa kijiji hicho kwa wageni, bila ya kushirikisha mkutano wa kijiji na fedha zinaingia mifukoni mwao.

Mkazi wa kijiji hicho, Salimu Mohamedi, alisema viongozi hao pia hawasomi mapato na matumizi ya kijiji na kijiji hicho kimekusanya mapato zaidi ya Sh milioni 14, lakini Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mtiti, Athumani Shabani, hasomi mapato na matumizi.

Kutokana na madai hayo, DC huyo ametoa wiki moja kuanzia sasa kuhakikisha ardhi hiyo inarejeshwa mara moja na kama hilo halitatekelezwa hatua zitachukuliwa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa