Home » » Waharibu miundombinu kabla ya kukamilika

Waharibu miundombinu kabla ya kukamilika


na Bertha Mwambela, Tanga
IKIWA imebaki miezi miwili  kabla ya kuzinduliwa barabara ya Tanga- Horohoro, watu wasiojulikana wameng’oa baadhi ya alama zinazoendelea kuwekwa katika barabara hiyo kunakodaiwa kufanywa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja wa Tanroads mkoani hapa, Alfred Ndumbalo, alisema kuwa wakati hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kuweka alama ambazo kitaalamu huitwa (roads making) zikiendelea  wapo baadhi ya wananchi wanazing’oa na kuuza kama bidhaa ya chuma chakavu.
Ndumbalo alisema vitendo hivyo vinatishia utunzaji wa barabara hiyo iliyokamilika kwa asilimia 96, hivyo kusababisha hasara kwa mkandarasi.
“Ifahamike barabara hii ni mali ya Watanzania hivyo tuna jukumu la kuitunza na kuilinda ili iweze kutumika kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo,” alisema meneja huyo.
Aliwataka wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo kushirikiana na wananchi kuhakikisha ulinzi shirikishi unafanyika ili kuweza kuinusuru barabara hiyo na kuhakikisha inatunzwa kama ilivyokusudiwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Naye mhandisi  wa mradi kutoka Wakala wa Barabara Mkoa,  Edward Nelson, alisema kuwa kwa sasa juhudi mbalimbali zimekwisha kutumika ikiwamo kutoa elimu kwa wanakijiji hao kuhusu matumizi sahihi ya barabara.
“Kwa sasa tumeandika barua ofisi ya mkuu wa mkoa na wilaya na kamanda wa polisi wa mkoa, kutumia kitengo cha usalama barabarani kutoa elimu kwa wananchi waishio pembeni mwa barabara hii ili wafahamu umuhimu wa alama hizi pamoja na matumizi sahihi ya barabara,” alisema Nelson.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa