Home » » Mara kinara kwa ukatili, Tanga yashika mkia

Mara kinara kwa ukatili, Tanga yashika mkia


na Rose Joseph, Musoma
UTAFITI uliofanywa na madaktari hapa nchini, unaonesha kuwa Mkoa wa Mara unaongoza kwa vitendo vya ukatili kwa asilimia 72, ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma wenye asilimia 71.
Utafiti huo uliohusu ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ulifanyika mwaka 2010 na kuonyesha kuwa Mkoa wa Tanga ndio wenye kiwango kidogo kabisa cha ukatili nchini.
Takwimu hizo zilitolewa jana mjini Musoma na daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, kutoka kitengo cha afya ya uzazi na mtoto cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Grace Mallya, wakati wa mkutano wa uhamasishaji viongozi wa mkoa na wilaya kuhusu mwongozo wa kisera na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, alisema vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu, vikiwamo vya kuwanyanyasa watoto kimwili na kingono kwa kuwalazimisha kufanya vitendo vya ngono bila ridhaa yao, usafirishaji wa wanawake na watoto kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono na kuwanyima haki ya kurithi mali za familia bado ni changamoto kubwa katika jamii.
“Kwa kuzingatia taarifa za utafiti, serikali imetengeneza mwongozo wa kisera na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili dhidi ya watoto, miongozo hii inatoa maelekezo pamoja na taratibu za kufuata katika kutoa huduma kwa watu walioathirika na ukatili wa kijinsia,” alisema.
Awali Kaimu Mratibu wa jinsia kitengo cha afya ya uzazi na mtoto, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Martha Rimoy, alisema Tanzania ni moja kati ya nchi 14 zilizofanya utafiti wa masuala ya ukatili katika Afrika na kubaini kuwa ina asilimia 44 ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa