Home » » Mafuta bandia yakamatwa, Muheza Tanga

Mafuta bandia yakamatwa, Muheza Tanga


na Bertha Mwambela, Muheza
NDOO 300 za mafuta ya bandia ya kula yaliyochakachuliwa yenye ujazo wa lita zaidi ya 600 ambayo ni hatarishi kwa afya za binadamu yamekamatwa wilayani Muheza baada ya kusambazwa kwa wateja tayari kwa kuanza kutumika.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi mkoani Tanga limewasilisha sampuli ya mafuta hayo kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) ambao nao watawasilisha sampuli hiyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo zaidi.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki wilayani Muheza ambapo mara tu baada ya kusambazwa kwa mafuta hayo kwa wenye maduka ya reja reja, baadhi yao walibaini mapema na kutoa taarifa polisi.
Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na limewatia mbaroni wafanyabiashara wawili walioingiza mafuta hayo huku taratibu za uchunguzi zikiendelea.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, waliotiwa mbaroni ni Khalid Abdallah na Saad Abdallah wote wakiwa ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Ndaki alisema kuwa baada ya mtego wa polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao katika eneo la Ubena wilayani Muheza.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji mkoa limewatia mbaroni Watanzania wawili wanaotuhumiwa kuwa ni mawakala wa kuingiza wahamiaji haramu kutoka nchi za Ethiopia na Somalia.
Watuhumiwa hao, Cleophace Isban na Daud James wanadaiwa kuhusika na kuwaingiza wahamiaji haramu 10 kutoka nchi hizo mbili ambao mpaka sasa bado wanashikiliwa na polisi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa