NA TIGANYA VINCENT
2 OKTOBA 2017
KUCHELEWA kupelekwa fedha ambazo zilitakiwa kwa ajili ya kuunga mkono
juhudi za wananchi ili waweze kukamilisha Mradi wao wa Ujenzi wa jengo
la Mashine ya Usindikaji wa Mafuta katika Kijiji cha Kombe umesababisha
Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kupewa wiki mbili
kuhakikisha fedha hizo zinafika haraka la sivyo atakuwa amejiundoa
kazini mwenyewe.
Msimamo huo umetolewa jana wilayani Kaliua na Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Mashine
ya kukamulia mafuata ya alizeti ambao umekwama kumalizika kwa zaidi ya
miezi mitatu baada ya Halmashauri kuchelewa kupeleka fedha ambazo
ilitakiwa itoe.
Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wananchi wamejituma kujenga
jengo kwa ajili ya kuweka mashine ya kusindika mafuta ya alizeti lakini
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua hadi hivi sasa hajitoa milioni 4
zilizotakiwa kuunga mkono nguvu za wananchi hao.
Aidha Mwanri aliongeza kuwa pia kiasi kingine ni zile milioni 17
zilizotolewa na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Miombo kwa ajili shughuli
mbalimbali kama vile ufugaji kuku, kilimo cha uyoga, ufugaji nyuki
zimekwama kupelekwa kwa walengwa kwa sababu ya Ofisi ya Uhasibu ya
Halmashauri hiyo kuchelewesha wakati Wilaya nyingine zimeshapeleka kwa
walengwa na kuanza kufanyakazi.
Alisema kuwa hawezi kumvumilia mtumishi wa sampuni hiyo ambaye
ameshindwa wa kutumia fedha miradi kwa wakati ambazo zimetengwa kwa
ajili ya kuwasaidia wananchi katika kuwainua kiuchumi na kuwaletea
maendeleo yao na taifa kwa ujumla kwa sababu ya urasimu usio na maana
kwani kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa.
Mwanri alisema kuwa ndani ya wiki mbili mbili anataka kupata majibu ya
hatua ambazo zimefikiwa katika kuhakikisha kuwa fedha hizo za mradi
endelevu wa miombo zimeshapelekwa eneo husika na Halmashauri ya Wilaya
ya Kaliua imeshawakabidhi wananchi hao milioni 4 ili wamalizie jengo la
mashine yao.
Mwanri alisema kuwa kinyume cha hapo wahusika wote watakuwa wamesbabisha mradi huo kutofanikiwa waanze kuondoka kwa hiari yao.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alitoa siku mbili kwa uongozi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuhakikisha wanapeleka taarifa ya
miradi yote inayotekelezwa na gharama zake na muda wa kukamilisha mradi.
Alisema kuwa hatua hiyo inataka kufanya Ofisi yake kuwa na uhakika wa
thamani halisi ya fedha na ubora wa mradi ili kuona kama kweli
utawanufaisha wananchi.
Naye Mratibu wa Mradi wa Miombo Wilayani Kaliua Bennett Kamara alisema
kuwa taratibu zote za kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa na miombo
zinatolewa na Mkurugenzi Mtendaji ili ziunge mkono juhudi za wananchi
zilishakamilika muda mrefu lakini kwa muda mrefu fedha hizo bado ziko
ofisi ya Uhasibu.
Kwa upande wa Katibu Tawala Msaidizi Dkt. Philip Ntiba alitoa wito kwa
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kutoa haraka fedha mapema ili
kuwakatisha tamaa wananchi waliojitolea nguvu zao kuanzisha mradi huo.
0 comments:
Post a Comment