Na Husna Saidi- MAELEZO
Serikali
kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeanza kazi ya
uboreshaji wa Reli ya Tanga ambayo ni moja ya chanzo cha kukuza uchumi
ili kuleta maendeleo ya nchi.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Edwin Amandus Ngonyani alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na
Mbunge wa Muheza Balozi Adadi Mohamed Rajabu wakati wa kipindi cha
maswali na majibu katika bunge la kumi na moja aliyetaka kujua kuhusu
suala hilo leo mjini Dodoma.
Mhandisi
Ngonyani alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Reli ya Tanga
katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini, tayari imeanza kufanya
usanifu na tafiti mbalimbali zitakazosaidia zoezi hilo kufanyika kwa
ufasaha.
“Mpango
wa Serikali uliopo ni kuunganisha Bandari ya Tanga na Bandari mpya ya
Mwambani kwenye Reli ya Standard Gauge ya Ukanda wa Kati kupitia Reli ya
njia panda ya Ruvu hadi njia panda ya Mruazi ambayo imeunganisha Reli
ya Kati na Reli ya Tanga hadi Arusha,” alisema Mhandisi Ngonyani.
Aidha
alisema kuwa usanifu wa kina wa Reli ya kutoka Tanga hadi Arusha yenye
kilomita 438 umekamilika hivyo kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta
fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ili kuanza ujenzi wa Reli hiyo
ya Tanga hadi Arusha kwa kiwango cha kimataifa.
Mhandisi
Ngonyani aliongeza kuwa Mhandisi Msaidizi, Kampuni ya HP Geult ya
Ujerumani inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kati ya
Mikoa ya Arusha na Musoma pamoja na matawi ya kwenda Engaruka na
Minjingu ili kuwezesha ujenzi huo kwa umakini.
Kufatia ujenzi wa Reli hiyo Serikali itafanikisha mpango mzima wa kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kupokea mapato yatokanayo na matunda ya Reli hiyo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment