Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo
Kikuu Ardhi kimekamilisha ujenzi na uwekaji wa vifaa katika Bandari ya
Tanga ikiwa ni moja ya miradi ya kiutafiti inayofanywa chuoni hapo kwa
ajili ya kupima hali halisi ya bahari.
Makamu
wa Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ameyasema hayo alipokuwa
akisoma hotuba wakati wa mahafali ya 10 ya chuo hicho yaliyofanyika jana
chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Prof.
Mshoro amesema kuwa pamoja na jukumu la kutoa wahitimu katika fani
mbalimbali kwa maendeleo ya nchi pia chuo hicho kina majukumu ya kufanya
utafiti na kutoa ushauri wa kitaalam hivyo kupitia Mradi wa Utafiti wa
Mabadiliko ya Tabia Nchi uliofadhiliwa na Serikali ya Norway kwa
kushirikiana na Serikali ya Tanzania umeweza kufanikisha ujenzi huo.
“Madhumuni
ya Mradi huu ni kusaidia kuboresha mawasiliano kati ya Bandari na
watumiaji wake kwani taarifa sahihi zitakazotolewa kuhusu hali halisi ya
bahari zitasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kutumia Bandari hiyo pia,
taarifa hizo zitakuwa msaada mkubwa kwa wadau wengine kama wavuvi,
watalii pamoja na watafiti mbalimbali,” alisema Prof. Mshoro.
Ameongeza
kuwa katika kutoa ushauri na huduma za kitaalam, chuo kimetekeleza
miradi mbalimbali ya Serikali, taasisi za Umma na Binafsi katika fani
zote zinazofundishwa chuoni hapo hivyo kusaidia katika kuongeza kipato
cha chuo kwa ajili ya miradi, kutoa motisha kwa wafanyakazi pamoja na
kutoa fursa kwa wana taaluma kupata uzoefu kwa vitendo katika fani
mbalimbali walizosomea.
Aidha,
Prof. Mshoro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea
kukipatia chuo fedha na misaada mingine kwa ajili ya kuendeshea shughuli
za chuo ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetengea jumla ya
shilingi bilioni 5 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya chuo hicho.
Akiongelea kuhusu wahitimu, Prof. Mshoro
amefafanua kuwa jumla ya wanafunzi 968 watatunukiwa shahada na
stashahada mbalimbali ambapo wanafunzi 868 watatunukiwa shahada za
awali, 80 shahada za uzamili, 14 watatunukiwa stashahada pamoja na
shahada za uzamivu kwa wanafunzi 6.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi
Stella Manyanya amesema kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wasichana
kujiunga na masomo ya sayansi kwani idadi imeonyesha kuwa wahitimu wa
kike ni 320 ambayo ni sawa na asilimia 33 ya wanafunzi wote hivyo ametoa
rai kwa wasichana kutumia fursa za kusomea masomo hayo bila kuogopa.
Mhandisi
Manyanya amewashauri vijana kujikita kusoma masomo yatakayowapelekea
kujiajiri wenyewe kuliko yale yanayohitaji kuajiriwa kwani njia hiyo
itasaidia kujikwamua kiuchumi kwa haraka na kuchangia katika maendeleo
ya taifa.
0 comments:
Post a Comment