Home » » DED kortini kwa kutishia kumuua trafiki

DED kortini kwa kutishia kumuua trafiki


MKURUGENZI Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga, Emmanuel Mkumbo (41) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kumtishia kumuua kwa bastola askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa na kuvunja sheria za usalama barabarani.
Mkumbo ambaye ni mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani jana na alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Agripinas Kimanze kutoka kwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Sunday Hyera, akisaidiana na Ediga Bantulaki.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka hao wa serikali, mshitakiwa huyo anakabiliwa na kesi mbili, ya kwanza ikiwa ni kesi ya jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 226 ya mwaka 2016 na ya pili ni kesi ya Usalama Barabarani kwa mujibu wa Kifungu cha 222.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 15, mwaka huu eneo la Mkambarani wilaya ya Morogoro katika barabara kuu ya Morogoro- Dar es Salaam wakati akiendesha gari aina ya Toyota Pajero lenye namba za usajili T 845 CTJ.
Kosa la kwanza linalomkabili Mkurugenzi Mtendaji huyo ni kujaribu kumtishia kumuua kwa bastola askari aliyejulikana kwa jina la Koplo Titunda, akiwa katika majukumu yake ya kikazi.
Makosa mengine ni kuendesha gari lenye namba T845 CTJ aina ya Toyota Pajero bila ya kuwa na leseni na kuendesha gari bila bima.
Hyera alidai kuwa makosa mengine ni mwendo kasi katika eneo lililoruhusiwa kuendesha mwendo wa spidi 50 kwa saa lakini alivuka na kufikia 85, kugoma kupeleka gari kituo cha Polisi na kuendesha bila uangalifu barabarani.
Mshitakiwa huyo alikana makosa hayo na kuachiwa kwa dhamana, huku kesi yake ikitarajiwa kufikishwa tena mahakamani Oktoba 31, mwaka huu.
Hata hivyo, jitihada za waandishi wa habari kupata picha halisi ya mtuhumiwa, hazikufanikiwa baada ya askari kumziba mtuhumiwa kwa koti pamoja na kofia aina ya pama na kumuingiza katika gari aina ya Toyota na kuondoka.

0 comments:

Post a Comment

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Tanga Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa