Shigela awatoa hofu wananchi bomba la mafuta
SERIKALI imewaondoa hofu wananchi ambao maeneo yao ya ardhi,
yatatumika kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika
Mashariki (EACOP).
Bomba hilo linaanzia nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga kwamba
sheria itazingatiwa ili kila mmoja aweze kulipwa fidia inayostahili.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela wakati
wa ziara fupi katika Kata ya Chongoleani. Alitembelea eneo hilo ili
kukagua eneo la ujenzi wa gati ambalo litatumika kupokea mafuta hayo
ghafi kabla ya kusafirishwa kwenda kwenye masoko ya kimataifa.
Alisema mpaka sasa mchakato wa utekelezaji mradi huo, unaokadiriwa
kugharimu zaidi ya Sh bilioni 4, unakwenda vizuri na kwamba wakati
watendaji wakisubiri muongozo utakaopitishwa kuhusu namna ya ulipaji wa
fidia kwa baadhi ya wananchi wa maeneo ya nchi za Tanzania na Uganda.
Mkoa wa Tanga umeanza kujiandaa kwa kusafisha eneo pamoja na
miundombinu ya barabara ili kuwezesha vifaa kufika kwa urahisi katika
eneo la ujenzi.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Msaidizi anayeshughulikia masuala ya
Petroli katika Wizara ya Nishati na Madini, Mwanaamani Kidaya alisema
ameridhishwa na maandalizi ya awali yaliyofanywa na uongozi wa
Halmashauri ya Jiji la Tanga.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment