Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wananchi wakiwa katika eneo la ajali katika
Kijiji cha Pangamlima wilayani Muheza, Tanga ambako lori aina ya Scania
lililokuwa linatokea Moshi kwenda Tanga mjini likiwa limebeba mchanga
kugongana uso kwa uso na basi la abiria la Simbamtoto kutoka Tanga
kwenda Dar es Salaam jana asubuhi. PICHA NA STEPHEN WILLIAM.
Watu 11 wamefariki dunia papohapo katika ajali
mbaya iliyohusisha basi la Simba Mtoto lililokuwa limejaa abiria
kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mchanga, katika eneo
la kijiji cha Pangamlima, kata ya Makole, wilayani Muheza, mkoa wa
Tanga.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 1:00 katika barabara kuu ya Tanga
-Segera, wakati basi hilo likielekea Dar es Salaam na lori likielekea
njia ya kwenda Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ajali hiyo, Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Tanga, Miyao Msikhela, alisema imehusisha basi la
kampuni ya Simba Mtoto lenye namba za usaji T. 393 DDZ, ambalo lilikuwa
likiendeshwa na Mwalimu Sheja na lori la mizigo aina ya Scania lenye
namba za usajili T 738 CFE ambalo lilikuwa linatoka Moshi kuelekea
Tanga mjini likiwa limebeba mchanga ambao ulitawanyika barabara baada
ya ajali.
CHANZO CHA AJALI
Alisema ajali hiyo ilisababishwa na dereva wa lori ambaye
lilimshinda na kuacha njia yake kulifuata basi la abiria na kugongana
uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 26.
Alitoa onyo kwa madereva wote kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani
ili kuepusha ajali za kizembe kama hizo na kusababisha vifo vya watu
wasio na hatia na vilema vya maisha.
MAITI ZAPELEKWA MUHEZA
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Elias Mayala, alisema walipokea maiti za watu 11waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Alisema maiti sita zimetambuliwa na ndugu na jamaa zao na tano bado
hazijatambuliwa na kwamba zimehifadhiwa katika chumba cha maiti
hospitalini hapo.
WALIOKUFA
Aliwataja waliokufa na kutambuliwa kuwa ni, Fred Venus, Mwalimu Mbwana, Sada Ally, Nagiris Hamisi, Raya Saidi na Mohamedi Saidi.
WALIOJERUHIWA
Mganga mkuu huyo wa wilaya aliwataja waliojeruhiwa katika ajali
hiyo kuwa ni, Erasto Mlinga, mkazi wa Dar es Salaam, Christian Nkoal,
mkazi wa Tanga mjini, Omar Mohamed, mkazi wa Zanzibar, Hussen Mabula,
mkazi wa Muheza, Kibibi Athumani, mkazi wa kijiji cha Kasanga na
Enocent Kileo, mkazi wa Moshi.
Wengine ni Makay Kitete, mkazi wa Tanga mjini, Hamza Sesige, mkazi
wa Kicheba, Muheza, Sharifa Hatibu, mkazi wa Masuguru, Muheza, Hamad
Mwinyi, mkazi wa Dar, Mussa Mohamed, mkazi wa Tanga, Abdallah Njama,
mkazi wa Makorora, Tanga na Masudi Khatumu, mkazi wa Chambageni, Tanga.
Wengine ni Haruna Waziri, mkazi wa Tanganyika, Muheza, Ally Juma
Iddi, mkazi wa Makanya, Same, Regina Robert, mkazi wa Tanga mjini, Dudu
Hassan, mkazi wa Tanga mjini na Dominicka Isack, mkazi wa Tanga mjini.
Pia wapo, Chrstina Robert, mkazi wa Same, Mustafa Mohamed, Mary
Kimasha, Marykioli Josephe, Hemed Said, Habudi Kilozo, Doto Andrea na
Samia Juma, wote wamelazwa katika Hospitali Teule Wilaya ya Muheza kwa
matibabu.
RAIS MAGUFULI ATOA RAMBIRAMBI
Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa
Tanga, Mwantumu Mahiza, kufuatia vifo vya watu 11 waliopoteza maisha
katika ajali hiyo.
Rais Magufuli pia amewapa pole ndugu, jamaa na marafiki wote
waliofikwa na msiba huo na amewataka kuwa wavumilivu na wastahamilivu
katika kipindi hiki kigumu.
"Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshituko mkubwa na kupitia
kwako Mkuu wa Mkoa wa Tanga napenda kuwapa pole nyingi wote waliofikwa
na msiba huu mkubwa na naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha
maombolezo," alisema Rais Magufuli katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari na kuongeza:
“Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na natoa pole kwa majeruhi wote walioumia katika ajali hii.”
Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wote wa barabara,
hususan madereva wa vyombo vya moto kuwa makini watumiapo barabara kwa
kuzingatia sheria zote zinazosimamia usalama barabarani ili kuepusha
ajali.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment