MOTO mkubwa umezuka
jana asubuhi katika eneo la Kivesa, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga,
baada ya lori la mafuta kuingia mtaroni na kumwagika mafuta ambayo
yalilipuka na kusababisha maafa makubwa kwa baadhi ya wakazi wa eneo
hilo.
Katika tukio hilo la kusikitisha, moto huo umeunguza nyumba tano, magari matatu, maduka 16, kuua kuku 32 na kujeruhi watu watatu baada ya lori hilo kupoteza mwelekeo wakati dereva wake akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki ya abiria ‘bodaboda’ na kujikuta akigonga nguzo ya umeme.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Flaisser Kashai, alisema limetokea saa tatu asubuhi wakati lori hilo aina ya Scania lenye namba T 870 BXB, mali ya Said Halifa, mkazi wa Handeni, kugonga nguzo ya umeme na kuingia mtaroni.
Alisema kutokana na moto huo kuwa mkubwa, gari la Kikosi cha Zimamoto, kutoka wilayani Korogwe, lilifika eneo hilo likitokea umbali wa kilomita 65; lakini wananchi walianza kulishambulia kwa mawe na kuvunja vioo vyote wakidai limechelewa kufika eneo la tukio.
“Baada ya lori hili kugonga nguzo ya umeme na kuingia mtaroni, mafuta waliyokuwa yakipelekwa Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, yalimwagika na kulipuka; hivyo ukaibuka moto mkubwa ambao ulisambaa mitaani.
Aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni pamoja na dereva wa lori, Ali Said (50), utingo wa lori hilo, Mohamed Ali (20) na Zubeir Saleh (24) na magari matatu kuungua moto.
“Ni jambo la kusikitisha gari lililotoka Korogwe zaidi ya kilomita 60 ili kuja kutoa msaada kupigwa mawe na kuharibiwa kabisa kwa kisingizio cha kuchelewa, kitendo hiki hakikubaliki kwani ni cha kihuni,” alisema Kamanda Kashai.
Aliongeza kuwa, majeruhi wote wamepelekwa Hospitali ya Bombo mkoani humo kwa matibabu zaidi.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment